Rais wa Iran, Hassan Rouhani  ameonya kuwa kama Marekani itafanya uamuzi wa kujiondoa kwenye makubaliano/mkataba wa usitishwaji wa programu ya nyuklia nchini humo, itajutia uamuzi huo.

Amesema kuwa amesikia tishio la Rais Donald Trump la kutaka kujitoa kwenye makubaliano hayo ifikapo Mei 12 mwaka huu na kwamba kama atafanya hivyo kitakachofuata yatakuwa ni majuto ya kihistoria.

Makubaliano hayo yaliyoingiwa mwaka 2015, yalihusisha Iran, Marekani, China, Urusi, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Kutokana na makubaliano hayo, Iran ilikubali kusitisha programu yake ya Nyuklia na ikaondolewa vikwazo vyote vilivyokuwa vimewekwa dhidi yake.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa nchi yake iko tayari kwa uamuzi wowote atakaoufanya Trump itakapofika Mei 12 na kwamba watajibu kwa namna yao.

Trump amekuwa akikosoa makubaliano hayo ya mwaka 2015 na kuyaita ‘makubaliano kichaa’, na ameahidi kuachana nayo.

Ufaransa, Uingereza na Ujerumani wamejaribu kumshawishi rais wa Marekani kuwa makubaliano yaliyopo hivi sasa ndio njia bora zaidi ya kuizuia Iran kuendeleza program yake ya silaha za kinyuklia.

Hata hivyo, Iran imeendelea kusisitiza kuwa mpango wake wa Nyuklia ni wa amani na umelenga katika kuwawezesha kupata nishati kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Wiki iliyopita, Israel iliibua kile ilichodai kuwa ni ushahidi wa nyaraka zinazoonesha kuwa Iran imekuwa ikitengeneza silaha za nyuklia tangu mwaka 2003 na kwamba hata baada ya kuingia makubaliano imekuwa ikiendelea na utengenezaji huo, hatua inayovunja mkataba.

Iran imekanusha vikali tuhuma hizo zilizotolewa na wahasimu wao wa muda mrefu.

Waliojihami kwa silaha wavamia kijiji na kuua makumi
Bodi ya mikopo kuanza kupokea maombi mwezi huu