Hatimaye Kocha Mzawa Mbwana Makata amerejea Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutangazwa kama Mbadala wa Kocha Charles Boniface Mkwasa aliyetangaza kujiuzulu kukinoa kikosi cha Ruvu Shooting.

Mkwasa aliyekuwa Kocha wa muda mrefu wa Ruvu Shooting alisitisha huduma yake klabuni hapo jana Jumatatu (Desemba 05), baada ya kuuandikia Barua Uongozi wa juu na kuthibitisha kujiuzulu kwake kwa shinikizo la kupata matokeo mabaya katika michezo mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.

Klabu ya Ruvu Shooting imethibitishja kumtangaza Kocha Mbwana Makata kuchukua nafasi hiyo, baada ya kukamilisha mazungumzo yaliyodumu kwa saa 24 zilizopita, na pande hizi mbili kukubaliana kufanya kazi kwa pamoja.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema wanaamini Kocha Makata atawavusha na kuirudisha timu yao katika mipango ya ushindi ili kumaliza Ligi Kuu msimu huu wakiwa mahala salama.

“Tunaamini Mbwana Makata ana uzoefu wa kutosha, atatuvusha hapa tulipo na kutupeleka katika mazingira mbayo tunastahili sisi Ruvu Shooting,”

“Tunaamini Makata ni Kocha sahihi ambaye ana kila sababu ya kuwa Ruvu Shooting katika kipindi hiki ambacho tumeamua kuachana na Kocha Mkwasa aliyetuandikia barua ya kujiuzulu jana Jumatatu,”

“Sisi kama Uongozi tunamtakia kila ma kheri Kocha Makata katika kazi yake na sisi kama Viongozi na hata wachezaji wetu tunaahidi kumpa ushirikiano mkubwa ,ili kufanikisha malengo tunayoyakusudia.” amesema Masau Bwire

Kabla ya kufungiwa na Kamati ya Maadili msimu uliopita, Kocha Makata alikua kikonoa kikosi cha Mbeya Kwanza FC ambacho kilishuka Daraja na sasa kinashiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Kabla ya hapo Makata alikua na Kikosi cha Dodoma Jiji FC ambayo aliipandisha Daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu Tanzania Bara misimu mitatu iliyopita.

Gabriel Jesus kuikosa Arsenal hadi 2023
ICC yapinga kuundwa Mahakama ya uhalifu wa Ukraine