Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela amewaagiza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Songwe kufanya ufuatiliaji wa wafanyabiashara wanaouza pembejeo feki za kilimo kwa wakulima.

Ametoa agizo hilo mapema katika kikao cha wadau wa Kahawa kanda ya Mbeya ambayo inajumuisha mikoa ya Songwe, Katavi, Rukwa na Mbeya.

Amesema kuwa kitendo cha mkulima kununua pembejeo feki ni kumsababishia umasikini mkulima huyo jambo ambalo halikubaliki katika Mkoa wa Songwe.

Aidha, amewaagiza pia Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha maafisa ugani wanakwenda kufanya kazi shambani kwa wakulima na sio ofisini, kwani kazi yao kubwa ni shambani.

“Kitendo cha mkulima wa Kahawa kupata robo kilo kwenye mche wa kahawa ni matokeo ya wataalamu wa Kilimo kutowatembelea wakulima mashambani, kwani wenzetu Kenya kwa mche moja wa Kahawa wanapata kilo sita hili suala haliwezekani, kwani sisi tuna ardhi nzuri yenye rutuba na watalamu wapo, hivyo nasisitiza tena watalamu wa kilimo kwenda shambani kwa wakulima,” amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela.

Pia amezielekeza Halmashauri zote kuhakikisha zinapanda miche laki mbili ya kahawa ili kuendeleza zao la Kahawa, kwani Kahawa ndio chanzo cha uhakika cha mapato kwa Halmashauri kwa sasa.

Kikao cha wadau wa Kahawa kwa Kanda ya Mbeya kina lengo la kuendeleza zao la Kahawa pamoja na kubadilishana uelewa juu ya mnada wa kahawa ambao utaanza kufanyika kikanda mwaka huu katika Mkoa wa Songwe kwenye Halmashauri ya Mbozi

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 15, 2019
Joshua Nassari avuliwa Ubunge

Comments

comments