Joto la pambano la Mzunguuko wa 33 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Namungo FC linaendelea kupanda huku siku mbili zikisalia kabla ya miamba hiyo kukutana uso kwa macho Uwanja wa Mabatini, Mkoani Pwani.

Mkuu wa Idara ya Habari ya ruvu Shooting Masau Bwire amesema maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri, na wamejizatiti kupata alama tatu ambazo zitawaongezea uzito katika Mshike Mshike wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Maandalizi yanaendelea kama kawaida na tupo tayari kwa mechi muda wowote, tumejipanga kuhakikisha hachomoki mtu katika mechi hizo lazima tuchukue pointi zote dhidi ya wapinzani wetu.”

“Tunafahamu hakuna mechi rahisi kwenye soka, hivyo ni wazi huu mchezo utakuwa mgumu kwa sababu kila mtu anataka hizo pointi ili iweze kuwa salama kwa upande wake, lakini na sisi kwa upande wetu tumejipanga vizuri sana,” amesema Bwire.

Ruvu Shooting inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku ikiwa imejikusanyia alama 38 katika michezo 32 na imeshinda 10, imepoteza 14 na sare nane.

Ruvu Shooting haina uhakika wa kubaki ndani ya ligi ikiwa itayeyusha alama zake sita kwenye michezo miwili iliyosalia, hivyo ina kazi ya kufanya ili kupata matokeo.

Pointi zake zinaweza kufikiwa na Coastal Union iliyo nafasi ya 17 na alama 34 baada ya kucheza michezo 32.

Baada ya mchezo huo, Julai 18 Ruvu Shooting itamaliza msimu uwanja wa nyumbani kwa kucheza dhidi ya Azam FC.

Rais Dkt. Mwinyi awaapisha Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu
Watanzania waaswa kushiriki Sensa ya watu na makazi 2022