Baada ya kumalizana na KMC FC katika mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana Jumanne (Oktoba 19), Uongozi wa Young Africans umetangaza mkakati wa kujiandaa na mchezo wa Mzunguuko wanne, dhidi ya Azam FC utakaochezwa Oktoba 30.

Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa kwa kufikisha alama 09, itakua wenyeji katika mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu Young Africans Senzo Mazingisa Mbatha amesema, baada ya kikosi chao kurejea jijini Dar es salaam leo Jumatano (Oktoba 20) kikitokea mjini Songea mkoani Ruvuma, moja kwa moja kitaingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam FC.

Amesema lengo kubwa ni kushinda mchezo huo, ili kutimiza mpango wa kuendelea kuokota alama tatu za kila mchezo, kama walivyodhamiria msimu huu, ili kufanikisha azma ya kurejesha heshima ya ubingwa wa Tanzania Bara, iliopotea kwa miaka mianne mfululizo.

“Tumemaliza mchezo salama, na tayari kikosi kimesharejea jijini Dar es salaam, kwa ajili ya maandalizi yetu na Azam FC, maana tunaona tutakuwa mchezo mzuri na wenye ushindani ila tumejipanga kushinda mchezo huo bila kuruhusu droo wala kufungwa.”

“Tuna imani na Kocha Mkuu na benchi lake la ufundi watafanya vizuri ili kutusaidia kuweza kupata matokeo ya uhakika katika mchezo huo muhimu, kwani tumepania kuifuta kabisa historia yakufungwa na Azam FC, japo mpira huwa hautabiriki, ili hatutaruhusi kufungwa,” amesema Senzo.

Katika mchezo wa mwisho Young Africans ilikubali kufungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, lililofungwa na Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Prince Dube msimu uliopita 2020/21.

Hatma ya Mbowe kujulikana leo
Tony Bennett aweka rekodi mpya Guinness