Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa Serikali imesema haipo tayari kuivunja Taasisi ya elimu ya watu wazima isipokuwa ipo tayari kupokea ushauri wa namna bora ya kuimarisha utendaji wa Taasisi hiyo.

Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuendeleza Taasisi hiyo kwani bado inahitajika kutokana na faida inayoleta kwa taifa kusaidia kutoa elimu kwa watu wazima ambao walikosa mfumo rasmi wa Elimu.

Akizungumza wakati akijibu Hoja za Wabunge na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Waziri wa Elimu Sayansi na Teknplojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa Bado Taasisi hiyo inahitajika hivyo Serikali inaangalia namna ya kuiboresha na si kuivunja kama ilivyopendekezwa.

“ Taasisi ya Elimu ilianzishwa kwa lengo la kutoa elimu kwa wale waliokosa katika mfumo rasmi na pia kutoa mafunzo endelevu hivyo bado kuna umuhimu wa kuendeleza Taasisi hii” Alisisitiza Prof. Ndalichako.

Akifafanua Prof. Ndalichako amesema kuwa Taasisi hiyo inaweza kuimarishwa zaidi ili kuendana na mahitaji ya sasa ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuimarisha na kukuza kiwango cha elimu nchini.

Akizungumzia mikakati yakuimarisha elimu nchini Profesa Ndalichako amesema kuwa kwa sasa Serikali inafanya ukarabati wa Shule Kongwe hapa nchini, vyuo vya Ualimu, na Ujenzi wa maktaba yakisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 2500 kwa wakati mmoja hiyo ikiwa ni sehemu ya miradi yakuboresha elimu inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii yalipendekeza kuwa TEWW ivunjwe ambapo Serikali imesema kuwa Bado Taasisi hiyo inahitajika na ina tija hivyo kitakachofanyika ni kuiboresha zaidi ili kukuza elimu hapa nchini na Si kuivunja kama ilivyopendekezwa.

Kamati ya kusimamia ngumi za kulipwa yapewa majukumu
Sanchez kupandisha mshahara wa David de Gea