Viongozi wa maandamano ya kupinga Serikali nchini Sudan wamesema kuwa Jumapili ya Pasaka watataja viongozi watakaounda Serikali ya mpito ya kiraia ili kuchukua nafasi ya utawala wa kijeshi uliopo.

Baraza la Kijeshi lililomuondoa madarakani na kumuweka jela aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al-Bashir limetekeleza sehemu kubwa ya matakwa ya waandamanaji hao ambao walianzisha vuguvugu lililosababisha kuondolewa kwa kiongozi huyo.

Hata hivyo, bado waandamanaji wamekuwa wakipinga uwepo wa utawala wa kijeshi wakitaka utawala huo kuhakikisha unawapa fursa raia kuunda Serikali haraka iwezekanavyo, vinginevyo wameapa kutoondoka kwenye mitaa ya Khartoum.

Maelfu ya watu walikusanyika katikati ya jiji la Khartoum jana baada ya ibada ya Ijumaa ambapo Shirika la Habari la Reuters limeeleza kuwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu vuguvugu la kumng’oa al-Bashir madarakani lilipoanza. waandamanaji hao walisikika wakipaza sauti wakidai “uhuru, amani na haki.”

Viongozi wa maandamano hayo wamekuwa wakieleza kuwa wanaamini Baraza la Jeshi kuwepo madarakani wakati huu ni sawa na upande wa al-Bashir kuendelea kuwa madarakani.

“Kama hatutabaki barabarani ina maana hakuna tulichofanya, tutaendelea kuwa hapa hadi Baraza la Kijeshi litakapoondoka pia madarakani,” Reuters wanamkariri Rania Ahmed, mmoja wa waandamanaji.

Umoja wa Wataalam wa Sudan ambao umekuwa ukiongoza maandamano hayo umesema kuwa Jumapili ya Pasaka majira ya saa Kumi na Moja jioni kwa saa za nchi hiyo, watatangaza Serikali ya kiraia kuliondoa jeshi madarakani.

“Tunachotaka Baraza la kiraia ambalo pia litakuwa na wawakilishi wa Jeshi kuingia madarakani kuchukua nafasi ya Baraza la Kijeshi,” Ahmed al-Rabia, kiongozi wa umoja huo wa wataalam unaoundwa na madaktari, wahandisi na walimu ameiambia AFP.

Auawa kwa tuhuma za ushirikina mkoani Kagera
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Aprili 20, 2019

Comments

comments