Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi ameeleza mpango wake wa kuachana na muziki alioufanya tangu miaka ya 1990.

Sugu ambaye ana historia ya kuwa msanii wa kwanza kurekodi albam ya hip hop ya Kiswahili kwa gharama ya juu zaidi ndani ya studio za Master Jay, amesema kuwa baada ya kazi hiyo ya muda mrefu, sasa anawaza kuachana na muziki ili afanye majukumu mengine.

“Lakini kuliko kuwa kimya bila kuwa ‘active’ kimuziki nadhani sasa nalazimika kufikia mwisho na soon nitaweka rasmi MIC chini. Umri nao unasonga na MAJUKUMU mengine yanayohitaji muda wangu zaidi yanaendelea kuongezeka kwa neema zake MUNGU,” Sugu ameandika.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, mbunge huyo ameandika mpango wake huku akijiuliza maswali kadhaa kuhusu namna na zawadi ipi itakuwa bora zaidi ya kuwaachia mashabiki wake.

“Suala ni FANBASE yangu naiagaje wakati utakapofika? Kwa ALBUM au just a CONCERT?!… #JONGWE #MVMP #PoliticalPrisonerNo219 #JongweMisuti #SiasazaMars,” ameeleza mbunge huyo.

Sugu ndiye msanii wa kwanza wa Hip Hop Tanzania kupata mafanikio ya kimuziki kupitia albam, ambapo mwaka 1995 albam yake ‘Ni Mimi’ ilipata umaarufu na kusaidia kupenya kwenye soko la muziki.

Mara ya mwisho, Sugu aliachia albam ya ‘VETO’ mwaka 2009, lakini amekuwa akitoa ngoma kadhaa moja moja ikiwa ni pamoja na ‘Freedom’.

Amekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini tangu mwaka 2010, na mwaka 2015 alikuwa Mbunge aliyeongoza kwa kupata kura nyingi zaidi kwenye uchaguzi huo.

Trump amvaa muigizaji wa ‘Empire’ akiwa Japan
Mvuvi aliwa na mamba Mto Mara

Comments

comments