Achana na Elius Maguli mfungaji namba moja wa timu ya Stand United, kiungo mshambuliaji, Suleimani Kassim ‘Selembe’ namtazama kama mchezaji muhimu zaidi katika timu hiyo.

Selembe amekwishacheza michezo yote 18 ya timu yake katika ligi kuu, amefanikiwa kufunga goli moja tu  lakini mchango wake ni mkubwa mno katika ufungaji kwani hadi sasa  amefanikiwa kupiga pasi nane ( 8) zilizozaa magoli.

Nimefanya mahojiano na mchezaji huyo leo Jumatatu na kikibwa nilitaka kufahamu mwendo wao wa kasi walioanza nao katika mzunguko wa kwanza umekwenda wapi.

“Mzunguko wa pili unakwenda safi, Mungu anasaidia. Tumepania kushika nafasi za juu msimu huu licha ya kwamba mzunguko wa pili umeanza kwa ugumu.” anaanza kusema mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Zanzibar.

“Ni kweli tulianza mzunguko wa pili kwa kasi licha ya kuwepo  kwa matatizo kadhaa katika uongozi. Tumepania kurudi katika kasi yetu katika mechi ijayo dhidi ya Simba siku ya Jumamosi.” anaongeza kusema Selembe mchezaji wa zamani wa Azam FC, African Lyon na Coastal Union.

Stand watacheza na Simba katika mzunguko wa 19 mwishoni mwa wiki hii na licha ya ushindi wa mechi tano mfululizo waliopata ‘Wekundu wa Msimbazi,’ Selembe anaimani wataimaliza timu hiyo ya Dar es Salaam ambayo iliwafunga goli 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.

“Tuna uwezo mkubwa wa kuisimamisha Simba, tena sana. Tupo vizuri kwa sasa hatuna matatizo ndani ya timu. Kikubwa niwaomba mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani kutupa sapoti.”

Azam FC: Si Rahisi Kubadilisha Mfumo Kwa Sasa
Court Zouma Kuzikosa Fainali Za Mataifa Ya Barani Ulaya