Klabu ya AS Roma imeripotiwa kufikia makubaliano na uongozi wa Arsenal kwa ajili ya kuendelea kumtumia kwa mkopo mlinda mlango kutoka nchini Poland, Wojciech Tomasz Szczęsny.

AS Roma waliwasilisha maombi ya kuendelea kumtumia Szczesny kwa mkopo, baada ya kumsajili kwa njia hiyo msimu uliopita, na alionyesha kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye michezo ya ligi ya nchini Italia pamoja na ile ya kimataifa.

Hata hivyo taarifa za awali zinaeleza kuwa, huenda klabu hizo zikazungumza kwa mara nyingine tena baadae mwaka huu, ili kuangalia uwezekano wa kuuziana moja kwa moja mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 26.

Szczęsny, alilazimika kuondoka kaskazini mwa jijini London mapema msimu uliopita baada ya kusajiliwa kwa mlinda mlango kutoka Jamuhuri Czech, Petr Čech akitokea kwenye klabu ya Chelsea.

Kusajiliwa kwa mlinda mlango huyo kuliifanya Arsenal kuwa na makipa watatu wenye uwezo unaoshabihiana, kwani tayari mlinda mlango kutoka nchini Colombia, David Ospina Ramírez alikua amesajiliwa mwaka mmoja nyuma.

Klopp Aeleza Sababu Za Kumtimua Kambini Mamadou Sakho
Pep Guardiola Ampiga Kibuti Vincent Kompany