Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kinatarajiwa kuingia kambini Kesho Jumamosi (Machi 18), tayari kwa maandalizi ya michezo miwili ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) dhidi ya Uganda ‘The Cranes’.

Stars itacheza dhidi ya Uganda Machi 24 katika mchezo utakaofanyika nchini Misri kabla ya kurudiana Machi 28, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo amesema kikosi cha Stars kitaingia kambini Machi 18, mwaka huu na kitasafiri kwa makundi kuelekea nchini Misri.

Amesema Kundi la Kwanza litaondoka Machi 19, mwaka huu na Kundi la Pili litaondoka Machi 20, mwaka huu baada ya mchezo wa Young Africans dhidi ya US Monastir kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ofisa huyo alisema maandalizi yote kwa ajili ya safari yamekamilika na anaamini kwa kikosi ambacho kimeitwa na mwalimu kitafanya vizuri, huku akiwaomba Watanzania kuipa sapoti timu yao iweze kufanya vizuri katika michezo yake hiyo miwili.

“Kikosi cha timu yetu kitaingia kambini Machi 18, mwaka huu, lakini kitasafiri kuelekea nchini Misri kwa makundi wakati Machi 19, litaondoka kundi la kwanza na Machi 20, litaondoka kundi la pili kuelekea nchini humo kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza,” amesema Ndimbo.

Wachezaji waliotwa kuunda kikosi hicho ni Aishi Manula (Simba), Beno Kakolanya (Simba), Metacha Mnata (Yanga), Kibwana Shomari (Yanga), Datius Peter (Kagera Sugar), Yahya Mbegu (Ihefu), David Luhende (Kagera Sugar) Dickson Job (Yanga), na Abdallah Mfuko (Kagera Sugar)

Wengine ni Bakari Mwamnyeto (Yanga), Ibrahim Baka (Yanga), Mudathiri Yahya (Yanga), Sospeter Bajana (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba), Yusuph Kagoma (Singida BS) na Ramadhani Makame (Bodrumspor-Uturuki).

Pia wamo Abdul Suleiman (Azam FC), Edmund Joh (Geita Gold), Fisal Salum (Yanga), Khalid Habibu (KMKM FC), Anuary Jabiri (Kagera Sugar), Simon Msuva (Al-Qadslah-Saudi Arabia), Mbwana Samata (KR Genk-Ubelgiji), Novatus Dismas (Zulte Waregem- Ubelgiji), Alphonce Mabula (FX Spartak Subotica-Serbia), Kelvin John (KRC Genk-Ubelgiji), Ben Starkle (Bastord United FC-Uingereza), Haji Mnoga (Aldershot Towan-Uingereza), Ally Msengi (Swallows-Afrika Kusini), Himid Mao (Ghazi El Mahallah SC- Misri) na Said Khamis (Al-Fujairah-UAE).

Tanzania inatafuta tiketi ya kucheza AFCON 2023 baada ya kushiriki Fainali hizo mara mbili mwaka 980 ilipata nafasi kwa mara ya kwanza katika fainali zilizofanyika nchini Nigeria huku 2019 ikicheza mashindano hayo nchini Misri.

Osimhen: SSC Napoli itatwaa ubingwa Ulaya
Mambo yameiva Ulaya, Robo Fainali UEFA