Uongozi wa Klabu ya Tanzania Prisons umetoa ufafanuzi wa suala la kuondoka kwa Kocha kutoka nchini Kenya Patrick Odhiambo, baada ya kuibuka kwa sintofahamu katika Mitandao ya kijamii.

Baadhi ya Mashabiki wa Soka la Bongo wanadai Kocha huyo amefukuzwa kufuatia kuandamwa na matokeo mabaya katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, wengine wakisema ameondoka kutokana na Mkataba wake kufikia kikomo.

Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu hiyo inayoongozwa na Jackson Luka Mwafulango imeeleza kuwa, Kocha huyo hajafukuzwa na badala yake ameshindwa kufikia makubalino ya kusaini mkataba mpya baada ule ya awali kufikia kikomo.

“Mkataba wa Patrick Odhiambo ulikuwa umeisha, lakini sababu kuu ya kuachana naye ni baada ya kutofikia makubalino ya kuongeza mkataba mpya.”

“Odhiambo atabaki kuwa Rafiki na Mwanafamilia wa klabu hii, kwa sababu tulikuwa naye tangu mwaka 2021 mpaka anaondoka hapa.”

“Katika kipindi hiki timu itakua chini ya Kocha Msaidizi Shaban Mtupa, huku harakati za kuongeza nguvu katika Benchi la Ufundi zikiendelea.”

Kocha Odhiambo ameondoka klabuni hapo, huku akiiacha Tanzania Prsisons ikiwa nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo 21.

Msimu uliopita Kocha huyo alikuwa na hali ngumu kufuatia kikosi chake kuingia katika michezo ya Playoff, lakini kilifanikiwa kubaki Ligi Kuu baada ya kuifunga JKT Tanzania ya Ligi Daraja la Kwanza (Championship) katika Michezo ya nyumbani na ugenini.

Kocha Coastal Union aomba muda
Jinsi ya kumthibiti mama mkwe mvunja ndoa