Rais wa Marekani, Donald Trump amesaini muswada wa sheria inayowaunga mkono waandamanaji wa Hong Kong chini China wanaodai demokrasia.

Sheria hiyo iliyopewa jina la ‘Human Rights and Democracy Act’ (Sheria ya Haki za Binadamu na Demokrasia) inaitaka Marekani kufanya mapitio ya kila mwaka kuona hali ya China Kidemokrasia na uhusiano wake na Marekani.

Trump amesema kuwa amesaini muswada huo wa sheria kwa heshima aliyonayo kwa Rais Xi Jinping, nchi ya China na watu wa Hong Kong.

Waziri wa mambo ya nje wa China, ametahadharisha kuwa kama Marekani itaendelea na mwenendo huo usio sahihi kwao watachukua hatua za haraka kujibu mapigo.

“Marekani imekuwa ikifanya kazi ya kupotosha umma na kutochukua taarifa za ukweli,” imeeleza taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya China.

“Imekuwa ikiwaunga mkono hadharani wahalifu ambao wamekuwa wakiharibu mali, kuchoma moto, kuwaumiza watu wasio na hatia na kuingilia sheria za nchi,” imeongeza.

Hata hivyo, mmoja kati ya wanaharakati wanaounga mkono maandamano ya Hong Kong, Joshua Wong amesema kuwa sheria ya Marekani ni hatua nzuri ya mafanikio kwa wakaazi wote wa jiji la Hong Kong.

Marekani na China zimekuwa katika vita ya kibiashara kwa muda mrefu. China imeeleza kuwa mwenendo wa Serikali ya Trump unaweza kuongeza ugumu wa hali ilivyo badala ya kutafuta suluhu.

Maeneo ambayo upinzani umeshinda Uchaguzi serikali za mitaa yawekwa wazi
Shomari Kapombe atakiwa kurudi Taifa Stars