Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini zikiwemo wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Chemba na Kondoa waliomsimamisha katika maeneo ya Chemba, Kalema, Bicha na Bereko akiwa njianu kuelekea mkoani Arusha kwa shughuli za kikazi.

Amesema Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Majaliwa amesema kwa sasa Serikali imeendelea na uchumbaji wa visima virefu, vifupi pamoja na kuweka mtandao wa mabomba ya kusamba maji katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na ya wilaya hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao.

Pia ameeleza kuwa wananchi wanatakiwa wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

Kufuatia hali hiyo Majaliwa amewaagiza watendaji wawachukulie hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.

Aidha, Majaliwa amezungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme, amesema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa huduma hiyo katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

Hivyo, ameagiza wakandarasi wamalize maeneo yaliyosalia katika REA awamu ya pili ndipo waendelee na awamu ya tatu. Alisema Serikali imetenga sh. trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na vya wilaya za Chemba na Kondoa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

 

Agizo la Serikali juu ya matibabu ya Lissu
Magufuli kujengea ukuta madini ya Tanzanite