Uongozi wa Pamba FC umewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo ya jijini Mwanza, kuelekea mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Bingwa mtetezi Simba SC.

Pamba FC iliyofunga safari kutoka Kanda ya Ziwa hadi Dar es salaam, itakuwa mgeni katika mchezo huo utakaoanza mishale ya saa moja usiku, Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Jumamosi (Mei 14).

Mwenyekiti wa Pamba FC Everist Hagila amesema, Uongozi wa klabu hiyo umekamilisha mipango na mikakati yote kuelekea mchezo wa kuikabili Simba SC kesho Jumamosi, na hakuna shaka yoyote ambayo itakua kikwazo kwao.

Hagila amesema mchezo dhidi ya Simba SC wanauchukulia kama mchezo wa kawaida, kwa sababu sheria za mchezo wa soka zitakazotumika kesho ndio hizo hizo zimekua zikitumika kwenye Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza ambayo wanashiriki msimu huu.

Amesema Pamba FC wanaona mchezo huo ni nafasi ya kipekee kwao kuhakikisha wanaondoka hapo walipo na kwenda katika hatua nyingine, kwa kutambua umuhimu wa michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ambayo kikanuni Bingwa wake hupata nafasi ya kuiwakilisha nchi Kimataifa.

“Tumejiandaa kikamilifu, Benchi la ufundi limefanya kazi yake ya kukiandaa kikosi kuelekea mchezo wetu dhidi ya Simba SC, sisi kama viongozi tumefanya kwa upande wetu ili kutimiza lengo linalokusudiwa.”

“Mchezo wa kesho una umuhimu mkubwa sana kwa Pamba FC kwa sababu ni nafasi ambayo itaweza kutuondoa hapa tulipo na kwenda katika hatua nyingine, michuano hii ni njia ya kutupelekea kimataifa, hivyo kama tutashinda na tukaendelea kufanya vizuri, tutakua klabu itakayopata mafanikio makubwa msimu huu.”

“Tumejizatiti kuhakikisha wachezaji wetu wanaionyesha dunia Pamba FC ni klabu ya aina gani, kwa hiyo ni kazi kwao kupambana na kutubeba sisi kama viongozi na wadau wengine wa klabu hii kupitia mchezo wa kesho.

“Tumewaahidi kuwa pesa itakayopatikana katika mchezo wa kesho dhidi ya Simba SC yote watachukua wao endapo watashinda na kutinga Nusu Fainali na hata ikitokea wamepoteza, kwa hiyo kazi imebaki kwao kupambana na kufikia lengo.” amesema Hagila

Mshindi wa mchezo wa kesho Jumamosi (Mei 14) atacheza hatua ya Nusu Fainali dhidi ya Young Africans iliyotangulia kwenye hatua hiyo kwa kuibamiza Geita Gold kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati.

Thadeo Lwanga: Nipo FIT kuikabili Pamba FC
Pamba FC kuishangaza Simba SC