Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa wafanyabiashara na wenye viwanda vya mafuta ya kupikia na sukari nchini kuhakikisha bidhaa hizo zinaendelea kupatikana katika maeneo yote na katika bei ya kawaida.

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatano, Mei 9, 2018) Bungeni Jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kutoa kauli ya Serikali kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia nchini.

“Natoa siku tatu kuanzia kesho Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi mafuta yote yaliyoko bohari yaondolewe yaendelee kusambazwa kama kawaida nchini kote ili kuondoa uhaba uliojitokeza na kamwe Serikali haitokubali kuchezewa na wafanyabiashara wasiowaaminifu,”amesema Majaliwa

Amesema kuwa kama uhaba wa bidhaa hiyo utaendelea, ifikapo Jumapili Serikali itaanza kufanya msako kwenye viwanda na maghala na kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuficha mafuta hayo.

Hata hivyo amesema kuwa takwimu zinathibitisha kwamba mafuta ya kupikia yaliyoingizwa nchini yanatosha, hivyo nchi haipaswi kuwa na uhaba. Amesema kwa mwezi mafuta yanayotumika nchini tani 28.9 na kila mwezi zinaingizwa tani 30,000.

“Hatuwezi kukubaliana na jambo hili kwa sababu haliko kwa bahati mbaya ni mpango uliopangwa kwani imekuwa ni kawaida kila tunapoelekea kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kunakuwa na upungufu wa bidhaa hasa sukari, hivyo Serikali haitakubali wananchi wateseke bila sababu za msingi,”amesema Majaliwa

Airtel yaja na Fursa ya wekeza na Airtel Money Branch
Video: Kauli ya serikali kuhusu sakata la mafuta ya kupikia