Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Idara ya Uhamiaji kuandaa semina za mafunzo ya elimu ya uraia kwa wahudumu ya hoteli na nyumba za kulala wageni nchini ili kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu.

Majaliwa ametoa kauli hiyo Januari 19, 2017 mara baada ya kuwasili katika Ikulu ndogo ya Njombe na kupokea taarifa ya mkoa wa Njombe iliyotolewa na mkuu wa mkoa huo, Christopher Ole Sendeka.

Katika taarifa hiyo Ole Sendeka amesema kwenye kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba, 2016 Idara ya Uhamiaji ilibaini kuwepo kwa raia 119 wa kigeni ndani ya mkoa huo, ambapo wahamiaji haramu 42 walikamatwa.

Waziri Mkuu alisema ni hatari kwa mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya raia wa kigeni walioingia nchini bila ya kufuata utaratibu hivyo aliitaka Idara hiyo ijipange vizuri ili kudhibiti watu wa aina hiyo.

“Anzisheni utaratibu wa kutoa semina kwa wahudumu wa hoteli na nyumba za kulala wageni. Hawa wakipata elimu ya uraia watawasaidia katika kutoa taarifa za kuwepo kwa wageni ambao wana mashaka na uraia wao,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mikoa kujikita katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma katika maeneo yao.

Amesema lazima kuwe na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika halmashauri nchini. “fedha hizo lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa yenye kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,”.

Aidha, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma kuibua maeneo mapya ya ukusanyaji wa mapato ambayo yatatumika katika utoaji wa huduma za jamii hivyo kuleta tija kwa Taifa.

Pia aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia vizuri miradi ya maendeleo inayojengwa katika maeneo yao kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na wasikubali kupokea miradi iliyojengwa chini ya kiwango.

Dimitri Payet Aondolewa Kundi La WhatsApp
Serikali kuboresha mradi wa maji Makambako