Uongozi wa Young Africans umempa siku 14 Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Haji Sunday Manara kuomba radhi kwa kosa la kuchezea Brand ya klabu hiyo.

Makamu mwenyekiti wa Young Africans Frederick Mwakalebela amemtaka Manara kufanya hivyo alipozungumza na waandishi wa habari leo mchana, Makao Makuu ya klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika mashariki.

Mwakalebela amesema endapo Manara atashindwa kufanya hivyo, taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, na tayari uongozi wa klabu hiyo umejiandaa kikamilifu kuendelea kuilinda Brand yake ambayo imetengenezwa kwa kipindi kirefu.

“Young Aficans ni klabu kongwe, na juzi tumetimiza miaka 86, tumetumia juhudi kubwa sana kutengeneza Brand ya klabu hii na sio kazi ndogo,”

“Hapa kati kati msemaji wa Simba SC kwa maana ya Haji Manara aliichezea Brand ya Young Africans, sisi kama uongozi tumechukua hatua za kisheria na taratibu zinazotakiwa,”

“Tumempelekea Demand Note kupitia kwa wanasheria wetu na tumempa siku 14 aweze kuja hadharani aombe msamaha, na kama itashindikana tutamfikisha mahakakani.”

“Tumetumia gharama kubwa sana kuhakikisha kwamba Brand yetu tunailinda na tunaikuza kila siku ya mwenyezi mungu, lakini sambamba na hilo anakuja mtu anaishusha Brand yetu na kuishusha thamani,”

“Kitu ambacho kimetuletea matatizo makubwa na wadhamini/ wafadhili, na pia hata biashara yetu ya jezi inakua inashuka na kuleta taharuki kwa wanachama wetu, hivyo niseme tumechukua hatua na tumeliomba shirikisho la soka nchini liweze kuchukua hatua.” Amesema Mwakeleba.

Manara aliweka picha ya jezi za Young Africans kwenye kurasa zake mitandao ya kijamii (Fecebook na Instagram) ambazo zilikua na maneno yaliyosomeka ‘VISIT KIDIMBWI’, ikwa ni saa chache baada ya Simba SC kusaini mkataba na Serikali ambao umewawezesha kuitangaza Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba wanaitangaza nchi kwenye michuano hiyo kwa kuvaa jezi zenye maandishi wa ‘VISIT TANZANIA’ ikiwa ni klabu ya kwanza nchini na Afrika Mashariki kufanya hivyo.

Sakata la Morrison, Mwakalebela aitaja TFF
Maalim Seif alikuwa kiongozi wa tofauti - Magufuli