Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo imetakiwa kuhakikisha inachambua na kufahamu bajeti za ushiriki za watanzania katika mashindano ya kimataifa mapema ili kuondoa hekaheka za mwishoni ambazo zinzawafanya washiriki kupunguza Ari ya ushindi.

Kauli hiyo imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan leo tarehe 27 Oktoba 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwapongeza washiriki wa mashindano ya Miss Kiziwi Afrika na Twiga Stars.

Rais Samia amesema ni vizuri Wizara ifanye mapitio ya kila hitaji la ushiriki huo mapema na kujua wapi zitapatikana pesa za kuwapeleka hao washiriki na kama kuna mapungufu ijulikane mapema.

Amelitaka pia Baraza la Sanaa kuwasimamia vizuri washiriki hao, huku akisema kutokana na ugumu wa lugha yao Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaandaa Vishkwambi vitakavyotumika kusaidia viziwi katika huduma za kijamii.

Nae raisi wa Chama cha Viziwi Afrika na Mwenyekiti wa Kituo cha sanaa na Utamaduni cha Viziwi Tanzania, Habibu Mrope amesema wakati wanatakiwa kwenda kushiriki mashindano hayo nchini Urusi walikosa fedha hadi walipoamua kumshrikisha Rais Samia na kuwasaidia.

Miss Kiziwi Tanzania Hadija Kanyama alifanikiwa kushiriki katika mashindano ya Afrika na kushika nafasi ya pili.