Katika kuelekea maadhimisho ya wiki ya Ubunifu yatakayofanyika jijini Dodoma Wadau mbalimbali wa maswala ya ubunifu wamekutana na kujadili kuhusu fursa , changamoto na matokeo ya jitihada mbalimbali zilizofanyika zenye lengo la kuleta matokeo chanya kwenye maswala ya ubunifu ,wadau hao ni pamoja UNDP ,UNCDF , Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH, na Mamlaka ya Masoko ya mitaji na dhamana .

Maadhimisho hayo yanayoendelea katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere JNICC mpka Mei 12, 2022, wadau hao wameelezea kuhusu hatua zinazochukuliwa na wabunifu kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha ubunifu unakuwa njia mojawapo ya kuleta maendeleo.

Ofisa kutoka COSTECH Promise Mwakale amesema kuwa COSTECH imeshiriki maadhimisho hayo kuelekea wiki ya Ubunifu kama wadau katika kufungua Masoko kwaajili ya Ubunifu.

“COSTECH imekuwa ikitoa ruzuku kwa ajili ya wabunifu na tunatoa ruzuku kuanzia kwenye mawazo na kuwakuza , kwa hiyo Kongamano hili ni muhimu kwetu kwani limejumuisha wadau wengine katika kufungua masoko na kuongeza mitaji kwa ajili ya wabunifu”Amesema Mwakale.

Naye Mkurugenzi wa Tafiti, Sera na Mipango katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) Alfred Mkombo amewaeleza wabunifu na wadau hao kuwa kazi yao ni kusimamia masoko ya mitaji kuhakikisha biashara zinazohitaji mitaji zinapata kupitia utaratibu uliopo.

“Leo tumekuwa na warsha ya kuangalia ubunifu katika maeneo ya biashara zinazoanza na biashara za kati kwamba namna gani hizi biashara zinapata mitaji kupitia masoko ya mitaji na sisi kama Mamlaka ya Masoko na mitaji tunasaidia ubunifu katika masoko ya mitaji.

“Kwa hiyo sisi tunawachagiza wananchi hasa vijana wawe wabunifu zaidi.Sasa hivi tuna mpango ambao tunafanya kwa ushirikiano na UNDP katika kutengeneza miongozo ya kusimamia mipango ya mitaji shirikishi.Tunaposema mitaji shirikishi ni utaratibu wa kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza mradi fulani unapata fedha,” Amesema Mkombo.

Aidha Mtalaamu wa Fedha kutoka UNCDF Paul Damocha amesema wao mbali ya kuwa moja ya wadhamini katika Wiki ya Ubunifu wamekuwa wakishiri katika kukuza na kuendeleza ubunifu kwa njia tofauti kwa kushirikiana na COSETCH, Serikali na wadau.

Amesema kuwa UNCDF kama wadau pia wanasaidia katika sekta ya fedha, sera na kutengeneza miongozo pamoja na kuelekeza idara za Serikali katika kutengeneza mazingira wezeshi kwa wabunifu na kuwapatia leseni.


Wanne Simba SC kuikosa Kagera Sugar
Angella na Harmonize watangaza balaa wimbo mpya