Mabingwa wa Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) Azam FC wanaendelea kuhangaikia mpango wa kuwarejesha nchini wachezaji wao saba wa kigeni, ili kufanikisha mpango wa kukiongezea nguvu kikosi chao.

Wachezaji hao ni Never Tigere, Donald Ngoma na Bruce Kangwa (Zimbabwe), Yakub Mohammed, Razack Abalora na Daniel Amoah (Ghana) pamoja na Nicolas Wadada (Uganda).

Wachezaji hao wamekwama katika nchi zao kutokana na uwepo wa zuio la kutotoka nje na kufungwa kwa mipaka kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.

Mkuu wa Idara Ya Habari Na Mawasiliano ya klabu hiyo, Thabit Zakaria amesema wakati wakiendelea na juhudi za kuwarudisha nchini, wanaamini kikosi kilichopo kitaweza kupambana katika michezo ya ligi kuu na kombe la shirikisho, kulingana na maitaji ya benchi la ufundi.

“Tunasubiri nchi zao zifungue mipaka, tumejaribu kila njia, tumeshindwa.”

“Sidhani kama tunaweza kufanya vibaya kwa sababu ya kutokuwepo kwa wachezaji hao, Azam kuna wachezaji wengi ambao wanaweza kuyabeba majukumu yao kulingana na maitaji ya benchi la ufundi, ” amesema afisa habari wa Azam FC, Thabit Zakaria.

Kukosekana kwa wachezaji hao kunaweza kuathiri ushiriki wa Azam katika michezo iliyobaki ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam ambalo wapo katika hatua ya robo fainali waliyopangwa kukutana na Simba, Julai Mosi.

Azam FC inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 54 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 51 wakati Simba wakiwa vinara na pointi zao 71.

Vingozi wa vijiji matatani baada ya polisi kukamata hekari 100 za bangi
Uchumi wa China waporomoka