Ushindi wa mechi nne mfululizo za mwisho za Simba haukwenda bure, badala yake umekuwa na faida mara mbili, ukiachana na kupata pointi tatu kwa kila mechi lakini mwisho wamefanikiwa kuchota jumla ya shilingi milioni 20.
Fedha hizo zimepatikana kwa kile kinachoitwa ni ‘bonus’ baada ya ushindi wa mechi zao dhidi ya Singida United, Mbeya City, Ndanda na Prisons ambapo katika mechi hizo kila mechi wachezaji hao walipewa milioni tano wagawane.
Mtu wa ndani kutoka Simba ameliambia gazeti hili kuwa, fedha hizo hugawiwa kwa asilimia tofauti kwa wale walioanza kwenye kikosi cha kwanza, walioingia kutokea benchi, ambao hawakucheza na hata wale waliokaa jukwaani.
Imeelezwa kwamba awali kulikuwa na kiwango kidogo cha bonus kinatolewa lakini sasa kimeongezwa na kufikia milioni tano katika mechi zilizofuata baada ya ile ya Yanga waliyofungwa 2-0.
“Hii mara nyingi hufanyika kwenye  mechi za Uwanja wa Taifa ambazo mara nyingi zimekuwa hazina mapato makubwa na tangu mpango huu uanze, mechi zote zimechezwa Dar.
“Sasa hii ya Coastal Union kwa kuwa mkoani kutakuwa na kiwango lakini bado hakijapitishwa moja kwa moja ni shilingi ngapi,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Meneja wa Simba, Abbas Ali kuzungumzia suala hilo, alisema: “Bonus zipo tangu mwanzo wa ligi mbona, ila timu ikifungwa haipati kitu na kama ikitoa sare kuna asilimia pia inapata ambayo ni tofauti na ikishinda.”
Wakati huohuo, kuna taarifa kuwa wachezaji wa Simba hawajalipwa mishahara ya mwezi uliopita. Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara kuhusu suala hilo alisema: “Siyo kweli kwamba wachezaji hawajalipwa, tatizo lililokuwepo ni mfumo wa kibenki umebadilika, hivyo fedha zinachelewa kuingia kwa wakati benki.”
Chanzo: CHAMPIONI
Simba avamia jiji la Nairobi na kujeruhi, ajiachia katikati ya foleni
Tanesco yamnyooshea mikono Magufuli, yatangaza haya