Mkurugenzi wa Sheria na Habari wa shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), Boniface Wambura ameupongeza Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kwa kufanya maamuzi ya haraka ya kumuajiri kocha Hitimana Thiery kukaimu nafasi ya Selemen Matola.

Simba SC ilimtangaza Hitimana Thiery mwishoni mwa juma lililopita, baada ya wa kuibuka kwa taarifa za Kocha Mkuu Didier Gomes kukosa sifa za elimu, ambazo zinatambuliwa na Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’.
Wambura amesema Uongozi wa Simba SC umefanya maamuzi mazuri ya kumuajiri Hitimana katika kipindi hiki ambacho ulihitaji kuwa na kocha mwenye vigezo vya CAF.

Amesema huenda hatua hiyo imechukuliwa tofauti na mashabiki wa soka nchini, lakini anaamini suala hilo kitaalum limekaa vizuri, hasa katika upande wa kuisaidia Simba SC kwenye michuano ya ndani na Kimataifa.

“Sio rahisi sana kama inavyochukuliwa na wengi walichokifanya Simba kumtafuta kocha wa kukaimu nafasi hiyo hawajakosea kwani kocha wao kozi yake ni ya mwaka mmoja na baadaye kupitishwa kama atakuwa amefanya vizuri.” amesema Wambura.

Tayari kikosi cha Simba SC kilichoweka kambi mjini Arusha, kimeshacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Fauntaine Gate na Eagle Noir ya Burundi chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Didier Gomes na Hitimana Thiery.

Jumapili (Septamba 19), Simba SC itacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya TP Mazembe katika uwanja wa Benjiamin Mkapa jijini Dar es salaam katika Tamasha ya Simba (Simba Day).

Kamwaga: Simba watajaza uwanja jumapili
Young Africans kuondoka ijumaa