Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ametoa wiki tatu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo waliopo ndani ya Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho vitakavyowafanya wambuliwe rasmi na serikali na hivyo kujulikana shughuli zao wanazozifanya katika maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa hiyo.

Ameyasema hayo katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa kata na mitaa ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ili kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano katika manispaa hiyo.

Amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuyatambua makundi yote ya wafanyabiashara nchini na katika kufikia lengo hilo imeweka utaratibu maalum wa kuwapatia vitambulisho wajasiliamali ili wasibughudhiwe, na kuongeza kuwa ili waweze kutafutiwa maeneo yao maalum ya kufanyia kazi ni lazima watambuliwe.

“Kama hana kitambulisho hiki ambacho amekitoa Rais na wakati huo huo hana TIN ya biashara ya TRA sasa yeye ni nani? Narudia kusema kwamba yeyote baada ya wiki tatu ambaye hana kitambulisho, hatauza hata nyanya nje ya mlango wake, kwasababu ni mfanyabiashara mdogo, na kama haupo kwenye ufanyaji biashara mkubwa wa kuwa na TIN na hauna kitambulisho cha ujasiliamali inamaana haufanyi shughuli za biashara,” Amesema Wangabo

Aidha, amebainisha makundi ambayo ni walengwa wa vitambulisho hivyo wakiwemo, mafundi baiskeli, wauza mkaa, wauza nyanya, wauza, vioski mitaani, mafundi seremala wa mitaani, mama ntilie, wauza matunda wa mitaani, waendesha bodaboda, pamoja na wale wote wanaojishughulisha na biashara ambao hawajafikia vigezo vya kusajiliwa na TRA.

Hata hivyo, Wangabo amewaonya wale wote wanaosita kuchukua vitambulisho hivyo wakidhani kuwa havina umuhimu na kwamba hakuna tofauti ya kuwa nacho na kutokuwa nacho wasubiri baada ya wiki hizo tatu kupita ndipo itajulikana umuhimu wa kitambulisho hicho.

 

 

Benki ya Dunia yatoa Bilioni 21.7 kuboresha miundombinu Mtwara
Mahakama ya ICC yamuombea hifadhi Gbagbo Ubelgiji

Comments

comments