Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema kuwa Benki ya CRDB ikiwa benki kinara katika uwezeshaji katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini inapaswa kuelekeza nguvu zaidi kwa wajasiriamali wadogo kwani kwa kufanya hivyo itasaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kujenga uchumi wa kati.
 
Ameyasema hayo mkoani Simiyu alipotembelea banda la Benki ya CRDB katika maonyesho ya kilimo maarufu kama Nanenane yanayoendelea mkoani humo.
 
“Kuna makundi ya wakulima wadogo, bodaboda, machinga na wajasiriamali wengine wadogo ambao wamekuwa wakisahaulika kutokana na kutokuwa na dhamana na mikopo yao inatolewa kwa riba kubwa. Niwaombe Benki ya CRDB mtengeneze mpango mkakati mzuri wakuyahudumia makundi haya kwa unafuu na tuelekeze nguvu zetu huku kwani hawa ni wengi zaidi,” amesema Mizengo Pinda.
 
Kwa upande wake Meneja Mahusiano wa Benki ya CRDB anayehusika na Mikopo ya Kilimo, Maregesi Shaaban amemhakikishia Waziri Mkuu mstaafu kuwa Benki hiyo imejipanga vilivyo kuhudumia wajasiriamali wadogo katika sekta zote kupitia huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na Benki hiyo.
 
“Kwa upande wa wakulima tumeanzisha akaunti za ‘FahariKilimo’ ambayo ni mahsusi kabisa kwa ajili ya wakulima, akaunti hii hufunguliwa bure na hakuna gharama za uendeshaji tukilenga kumpa mkulima unafuu wa kupokea malipo pindi anapouza mazao yake” amesema Maregesi.
 
Aidha, Maregesi amesema kuwa Benki hiyo ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mikopo maalum kwa ajili ya wamachinga inayolenga kuwapa uwezo wa kukuza biashara yao kwa kuwapa mitaji.
“Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli amefanya jitihada kubwa sana na za kupongezwa katika kurasimisha kundi hili la wajasiriamali, hivyo kuunga juhudi hizi Benki ya CRDB ipo katika mchakato wa kuingiza mikopo maalum kwa ajili ya wamachinga huku vitambulisho vyao vikitumika kuwatambulisha” amesisitiza Maregesi.
Mapema kabla ya kutembelea banda la Benki ya CRDB, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alifungua semina maalum kwa wajasiriamali iliyoandaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) katika maonyesho hayo ya Nane nane yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu.
Mbunge atimuliwa kwa kuingia bungeni na mtoto wa miezi mitano
Video: Wananchi Kagera wafanya unyama wa kutisha