Baada ya kumpa mapumziko hadi mwishoni mwa msimu huu Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison, Uongozi wa Klabu ya Simba SC umetangaza kuwa kwenye mpango wa kusaini mikataba mipya na baadhi ya wachezaji klabuni hapo.

Simba SC ina wachezaji zaidi ya watano wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu, hivyo baadhi yao wataendelea kuwepo na wengine watafungashiwa virago kwa mujibu wa ripoti ya Kocha Mkuu Franco Pablo Martin.
Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Barbara Gonzalez amesema kabla ya kishindo cha usajili wa nyota wapya mwishoni mwa msimu huu, kwa sasa wanajipanga kuongeza mikataba ya waliopo kikosini.

Barbara amesema kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa kwenye viwango bora na kutoa mchango kwa ajili ya timu kuhakikisha inafanya vizuri, ni ngumu kuachana nao mara baada ya mikataba yao kumalizika.

“Halitakuwa jambo zuri kwa wachezaji wetu kuona wapya wanasajiliwa wakati wao walio kwenye kuipigania timu kufanya vizuri mikataba yao inamalizika na hawajasaini mikataba mipya.”

“Tutaanza kwanza na kuwaongeza mikataba wachezaji muhimu ambao mwisho wa msimu huu inamalizika na baada ya kumalizana nao, hapo tutaangalia mahitaji mapya ya timu kwa kumsikiliza kocha.”

“Wakati huu nimetingwa pamoja na kuzidiwa na majukumu mengi kuhakikisha tunakamilisha zoezi hilo la kuwaongeza mikataba mipya wachezaji wetu na baada ya hapo akili itatulia kufanya mengine yafuatayo.” amesema Barbara

Kwenye kikosi cha Simba SC wachezaji wanaomaliza mikataba mwisho wa msimu huu ni Erasto Nyoni, Joash Onyango, Chriss Mugalu, Aishi Manula, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Pascal Wawa na Meddie Kagere.

Thobias Kifaru afichua siri nzito Mtibwa Sugar
Mwanasiasa aliyetekwa apatikana akiwa amefumbwa macho