Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich leo wametangaza kumsajili winga wa zamani wa Arsenal, Serge Gnabry.

Taarifa iliyoweka kwenye mtandao wa Bayern Munich imeeleza kuwa Gnabry mwenye umri wa miaka 21 amesaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Werder Bremen kwa ada ya Euro Milioni 8.

Gnabry alijiunga na Werder Bremen msimu uliopita baada ya kushindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha Arsenal kinachonolewa na Mfaransa,Arsene Wenger.

Akiwa na Werder Bremen msimu uliopita Gnabry aligeuka staa mkubwa baada ya kuifungia timu hiyo mabao 11 katika michezo 27 ya ligi ya Bundesliga.Mabao 10 kati ya 11 aliyafunga kwenye viwanja vya ugenini.

Pia aliibuka mfungaji kwenye michuano ya Olimpiki ambapo alifunga mabao sita na kuiwezesha Ujerumani kushika nafasi ya pili nyuma ya Brazil waliokuwa mabingwa.

Gnabry anakuwa mchezaji wa tatu kujiunga na Bayern Munich katika kipindi hiki cha majira ya joto.Wengine ni Sebastian Rudy na Niklas Süle.

Video: Majaliwa awavalisha vyeo Maafisa wa Magereza, ahimiza haki na usawa
Magazeti ya Tanzania leo Juni 13, 2017