Uongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto umefanya mabadiliko ya kitengo cha ujenzi kwa kukisuka upya ili kuweza kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya sita katika kusimamia miradi ya ujenzi.

Akiongea na waandishi wa habari leo ofisini kwake jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Abel Makubi amesema maamuzi hayo yamekuja kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya ukaguzi wa jengo la hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha, Menejiment ya Wizara imeona ni vyema hatua za haraka zichukuliwe za kujenga upya kitengo hicho na kuelekeza ofisi ya Sera na Mipango kuongeza kasi ya Uwajibikaji.

“Tunakibadilisha kitengo hicho na kuleta watu wapya ili kuleta ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya wizara husuan ile ya ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa ambapo ujenzi wake umekua ukisuasua na hivyo kutokamilika kwa wakati. Watalaamu wa kitengo hiki wameshindwa kujituma na kukosa ubunifu katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ujenzi” Aliongeza Prof.Makubi.

Prof. Makubi amesema kuwa wameshafanya tathimini ya miradi yote ya wizara ambayo imekua ikiendelea nchi nzima na kuona imekuwa ikichukua muda mrefu kutokamilika hilo ndilo lililafanya kukisuka upya kitengo hicho.Aidha Prof Makubi amesema watalaamu wa kitengo cha Ujenzi wameshindwa kuwa na usimamizi wenye matokeo na kushindwa kushauri haraka pale palipo na mkwamo.

Amesema wizara yake haiwezi kuvumilia tena kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi hiyo na hivyo kuwataka wale wote watakaoletwa wizarani hapo kutambua miradi yote inakamilika kwa wakati na lazima thamani ya fedha ionekane.

Waziri Mkuu Mhe.Kassimu Majaliwa mnamo tarehe 27 Agosti mwaka huu alifanya ziara na kukagua ujenzi wa hospitali hiyo na kuagiza Wizara ya Afya kurejesha usimamizi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa ofisi ya Mkoa , ambapo wizara ya afya tayari imeshatekeleza agizo hilo kwa kuzirejesha hospitali zote za rufaa za mikoa kwenye usimamizi wa Makatibu Tawala wa Mikoa.

Ibada maalumu ya kuwaombea Hayati Magufuli, Mkapa
Moto watekekeza wafungwa gerezani