Hatimaye uongozi wa klabu ya Yanga SC umeamua kumrejesha kocha wake Hans Van Der Pluijm kuendelea na nafasi ya ukocha mkuu katika klabu hiyo, ikiwa ni siku tano tangu aandike barua ya kujiuzuru.

Hayo yamefikiwa leo baada ya kikao cha pamoja kati ya uongozi wa klabu ya Yanga na Hans Van der Pluijm kilichofanyika katikati ya jiji la Dar es salaam. Kikao hicho kimefikia muafaka na Mdachi huyo kuendelea na kandarasi yake.

Kocha Hans raia wa Uholanzi aliyeishi Afrika kwa miaka zaidi ya miaka 18, aliandika barua ya kujiuzuru siku ya Jumatatu, kufuatia kutofurahishwa na kitendo cha uongozi wa klabu ya Yanga kumleta kocha wa Zesco George Lwandamina na kufanya nae mazungumzo ya kuchukua nafasi yake bila kumshirikisha.

Mtazamo wa wapenzi, wanachama wa klabu hiyo ulikua tofauti na zaidi ukipinga kuondolewa kwa kocha huyo, ili hali rekodi yake ikiwa ni ya kiwango cha juu katika michuano ya Ligi ya Kuu Tanzania, Kombe la FA, na Kombe la Shirikisho Afrika.

Uongozi baada ya kuona haukumtendea haki kocha Hans, leo umekutana na kocha huyo na kufikia muafaka wa kumrejesha kazini kuendelea na kibarua chake.

Kurejea kazini kwa Hans kunamanisha mipango ya kumleta kocha George Lwandamina kuchukua mikoba yake mwezi ujao kusitishwa, na sasa uongozi umeahidi kumpa ushirikiano wote kocha Hans katika kuhakikisha anatetea Ubingwa wa Ligi, Kombe la FA na katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

Usingizi wamzidi nguvu Rais Zuma bungeni
Mashabiki Wa Chelsea FC, West Ham Utd Kuchunguzwa