Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara umesema umekamilisha maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger kutoka Algeria utakaochezwa keshokutwa Jumapili (Mei 28) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Afisa Habari wa Young Africans Ali Kamwe, amesema kikosi chao kinaendelea vizuri na mazoezi na wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili kuimaliza mechi hiyo hapa nyumbani.

Kamwe amesema wakati benchi la ufundi likiendelea na majukumu yao, viongozi leo watakuwa na shangwe la fainali hizo kwenye viwanja vya Zakhiem, Mbagala, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhamasisha kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo.

“Hii ni mara ya kwanza kucheza fainali, viongozi wako makini sana na kutuliza akili ili kufanikisha malengo yetu ya kushinda nyumbani na kupata matokeo ugenini ili Juni 4, mwaka huu turudi na Kombe la Afrika,” amesema Kamwe.

Ameongeza kwa sasa wanatarajia kupata wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali huku CAF pekee ikileta maofisa wake zaidi ya 200.

“Sasa twende zetu Algeria na lengo kubwa kutafuta mashabiki kwenda nao na utaratibu ni ule ule wa awali wa kucheza bahati nasibu ili kupata nafasi ya kwenda nchini humo,” alisema msemaji huyo.

Naye Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki wa Young Africans, Haji Mfikirwa, amesema huu ni wakati mahususi kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao.

Mfikirwa amesema wamepokea tiketi nyingi tofauti na awali ambazo walikuwa wanapata katika michezo ya nyuma walipokuwa wakifanya harambee.

“Hadi sasa tumepokea jumla ya tiketi 18,213 kutoka kwa wadau mbalimbali akiwamo Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu, na tumeanza mchakato wa kuzigawa kwa wanafunzi wa vyuo na nyingine tunasubiri utaratibu mwingine wa kuwafikia wanachama wetu na mashabiki,” amesema Mfikirwa

Halmashauri kutoidhinisha maombi Watumishi wanaohama
Wakurugenzi kamilisheni miradi kwa wakati - Senyamule