Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli, amesema klabu yao iko tayari kufanya mazungumzo na timu yoyote ndani au nje ya Tanzania ambayo inahitaji huduma ya Kiungo hutoka nchini Uganda Khalid Aucho.

Kauli hiyo ya Bumbuli imetoka kufuatia tetesi zinazoendelea katika mitandao ya kijamii zikieleza kuwa, huenda Khalid Aucho akaondoka katika kipindi cha Dirisha Dogo la usajili ambalo rasmi litafunguliwa Desemba 15.

Bumbuli amesema Young Africans bado ina mkataba na Aucho, lakini inakaribisha ofa kutoka kwa timu yoyote na inawakumbusha viongozi wa klabu nyingine kufuata taratibu na si kutumia njia za ‘panya’.

“Tunasikia maneno maneno tu huko, lakini niwaambie tu Aucho ana mkataba wa miaka miwili na Yanga, tunafahamu huyu ni mchezaji mzuri na zipo timu zinamtolea macho, tunawaambia tu walete ofa yao tuone tunafanyaje, huyu ni mchezaji wa Yanga,” amesema Bumbuli.

Katika hatua nyingine Bumbuli amewataka Wanachama na Mashabiki wa Young Africans wasiwe na hofu yoyote juu ya kumpoteza mchezaji huyo kwa sababu bado ni mali yao kwa mujibu wa mkataba ambao alisaini na klabu hiyo.

“Unajua kila tunapoelekea kwenye dirisha la usajili, maneno mengi yanatokea, mashabiki wetu wasishtushwe na kelele hizi, wachezaji wote wana mikataba na hakuna mchezaji atakayeondoka kiholela,” amesema Bumbuli.

Sakata la Chama lafikia patamu
Aucho: Sina mpango wa kuondoka