Nahodha na Beki wa Young Africans Bakari Mwamnyeto, amewahakikishia Wanachama pamoja na Mashabiki klabu hiyo kuondoa hofu, kwani wanakwenda Algeria kulipa kisasi dhidi ya US Alger sambamba na kubeba Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Jumamosi (Juni 3), mwaka huu, timu hizo zinatarajiwa kuvaana katika mchezo wa mkondo wa pili wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa nchini Algeria.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Young Africans ilifungwa mabao 1-2, hivyo inahitaji kupata ushindi wenye wastani. wa mabao 2-0 ili kubeba ubingwa.

Mwamnyeto amesema anaamini mchezo utakuwa mgumu, lakini hiyo haiwafanyi waingie kinyonge, zaidi watapambana kupata ushindi mkubwa wa mabao.

Beki huyo aliyesajiliwa Young Africns miaka miwili iliyopita akitokea Coastal Union amesema, maandalizi waliyoyafanya yanatosha kabisa, wao kupata ushindi na kuandika historia ya kubeba kombe hilo.

Ameongeza kuwa, morali ya wachezaji ipo kubwa kambini na kila mmoja ameahidi kupambana kufa au kupona ili kupata ushindi.

“Kama wao walitufunga hapa nyumbani, basi sisi hatushindwi kuwafunga tutakapokuwa kwao.

“Kocha ameangalia upungufu na ubora wa wapinzani wetu wanapokuwa wanacheza mechi za nyumbani, hivyo tunaamini tutafanya vizuri,” amesema Mwamnyeto.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, amesema: “Tunakwenda ugenini baada ya wao kupata ushindi kwetu, tunaamini tumekuwa tukifanya vizuri kwenye mechi za ugenii, hilo linatupa nguvu ya kuamini kwamba tutafanya vizuri.”

Naye mshambuliaji wa timu hiyo, Fiston Mayele ambaye ni kinara wa mabao Kombe la Shirikisho Afrika akiwa nayo saba, amesema: “Tunafahamu huu ni mchezo ugumu kwa kuwa ni fainali na tunacheza dhidi ya timu ngumu ambayo imepata ushindi ugenini.

“Lakini kama timu tayari tumesahau matokeo ya mchezo uliopita na tupo tayari kupambana kushinda mchezo huu wa ugenini, tunachoomba ni mashabiki wetu kuendelea kutuombea kheri tuwe salama mpaka siku ya mchezo.”

Wanawake Halmashauri 184 nchini wapokea zaidi ya Bilioni 30
Polisi wafukua kaburi uchunguzi kifo tata cha Ester