Bertina Mangosongo – Mikumi.

Usanifu wa Daraja la kudumu la chuma (Mabey Bridge), litakalojengwa ili kuunganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo vilivyopo Kata ya Ulaya-Mikumi Wilayani Kilosa, umeanza.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini – TARURA, Mhandisi Victor Seff ameyasema hayo wakati akiongea na Wananchi wa kata hiyo kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya miundombinu wilayani Kilosa.

Akiwa katika eneo hilo, amemuelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro kuanza mara moja ujenzi wa Daraja la watembea kwa miguu (Kiteputepu), ili wananchi wa vijiji hivyo waendelee kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Aidha, Mhandisi Seff pia ameelekeza kufanyika kwa tathimini ya uharibifu wa barabara za Mikumi  ili ziwekwe kwenye mpango wa dharura wa kurudisha mawasiliano haraka iwezekanavyo.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Mikumi ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge – TAMISEMI, Dennis Londo amesema barabara nyingi za Jimbo la Mikumi  zimeharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha .

Daraja la watembea kwa miguu katika mto Nyali ambalo linaunganisha  vijiji vya Nyali na Nzumbo litajengwa kufuatia lile la awali kuvunjika.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 30, 2024
Mashujaa FC yaweka rekodi Ligi Kuu