“Naomba maji ya kunywa,” aliongea huku akitoa Sigara yake mfukoni na kuanza kuvuta kisha akasema “kama baba yangu kawafanyia mabaya ndugu zake basi ikiisha hii sigara niuweni,” ilipoisha akauawa kwa risasi ya shingo.

Anaitwa Mutassim Gaddafi, ni mtoto wanne wa Hayati Muammar Gaddafi aliyekuwa kiongozi wa Taifa la Libya aliyezaliwa mwaka 1974 Jijini Tripoli, akiwa mmoja kati ya watoto ambao Gaddafi aliwapenda sana kiasi cha kumpa cheo kikubwa Jeshini kati ya mwaka 2008-2011.

Kwa mwezi matumizi ya kawaida yalikuwa ni Bil. 3 na starehe yake kubwa ilikuwa ni Wanawake huku ikidaiwa kuwa aliwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Beyonce.

Alimiliki Ndege yake Binafsi, majumba ya kifahari na pia inadaiwa alikuwa na michepuko miwili Ulaya ambayo aliijengea  Maghorofa ya kifahari lakini hata hivyo, mwisho wake ulikuwa mbaya kwani aliuawa kifedheha na kuzikwa kusikojulikana Jangwani.

Mutassim alikuwa ni kijana wa kileo Vijana wa sasa wanaita ‘Bishoo’ yaani ni Mwanajeshi lakini ukimuangalia ni kama muigizaji wa filamu za Kihindi, na kutokana na kupendwa sana na Baba yake baadaye alikuwa mshauri binafsi wa masuala ya Usalama wa Gaddafi.

Mwaka 2005, akiwa kijana wa miaka 31, akanunua ndege yake binafsi (Private Jet), licha ya kuwa na umiliki magari mengi ya kifahari, alikuwa akivalia mavazi nadhifu sana huku shingoni na mikononi akivaa vito vya thamani ikiwemo Almasi na Dhahabu pekee, hakuwahi kuvaa ‘magoroka’.

Miaka ya 2000 kulikuwa na simu aina ya BlackBerry, Hizi simu zilikuwa na bei ghali sana, Sasa jamaa akatengenezewa ya kwake tena kwa oda maalumu ya dhahabu na inadaiwa alipenda sana Wanawake ikitajwa kama ndiyo ilikuwa starehe yake kubwa ana kwamba michepuko miwili nchini Uingereza na Italia.

Wanawake hao wakati wanahojiwa na Jarida moja mwaka 2012, kwa nyakati tofauti walikiri kuumizwa na kifo cha Mutassim kwani walikuwa wakiishi maisha mazuri enzi za uhai wake na walibahatika wote wawili kujengewa nyumba na kununuliwa magari ya kifahari na mmoja wa wanawake hao ni Vannesa Hessler ambaye alikiri kuwa kwenye mahusiano na Mutassim kwa miaka minne.

Mutassim alikuwa ni mtu viwanja vya starehe, kwani katika nyakati tofauti kila ifikapo mwisho wa mwaka alikuwa akienda Visiwa vya Caribbean na shuhuda mmoja wa kike aliowahi kuwa nae aitwaye Talitha Zion kutoka Ujerumani, anasema walipokuwa wakienda kwenye Hoteli kubwa barani Ulaya, Mutassim alikuwa akilipia vyumba vyote.

Talitha anasema, hakuwahi kufikiria siku moja kukutana na Mwanamuziki Mariah Carey kwenye ‘Private Party’ ya mwaka mpya wa 2008, ambapo Mariah alialikwa akitumbuiza na kwa mujibu wa mtandao mmoja, uliandika kuwa Mariah alilipwa dola milioni 9.5 kwa ajili ya onesho hilo.

Mwaka 2009 Mutassim alimualika, Beyonce kutumbuiza kwenye ‘Private Party’ Visiwani vya Caribbean na inaarifiwa kuwa alimlipa Dola Milioni 2 na siri nyingi za kuwatumia mastaa wakubwa duniani, ilikuwa ni kujijengea umaarufu akidai anafuta dhana kwamba Afrika ni Bara masikini.

Tom Groves alikuwa ni mpiga picha na mtu wa Mahusianokatika Klabu moja ya usiku ya St. Barts, yeye ndiye aliyetoa siri nyingi za Mutassim za jinsi alivyokuwa akijivinjari akisema kwa miaka mingi alimfahamu Mutassim na hakutaka hata Boss wa ile klabu amjue.

Anasema alitumiwa barua pepe na Mutassim akitaka kukodi klabu yote Siku ya mwaka mpya 2009 hakuamini, lakini akamuambia inabidi alipie malipo ya awali ya Dola laki 5 akijua fika kuwa hawezi kulipia fedha hiyo, akijua kwamba huyo ni mtu kutoka Afrika lakini Mutassim hakuomba hata punguzo akamtumia muda huo huo, hakuamini.

Anasema katika onesho hilo, alikuja Mwimbaji Beyonce na hakukuwa na tangazo lolote hakuamini yeye kama mualikwa na mtu wa PR klabuni hapo aliingia na kushangaa kumuona Beyonce akitumbuiza na kupiga picha na wageni waalikwa na kila mgeni alipewa chupa kubwa ya shampeni na bahasha ya mwaka mpya kama zawadi.

Tom anasema siku hiyo pia Wageni waalikwa walikuwa ni 150, wakiwemo watu maarufu kama Jay-Z, Usher Raymond, Lindsay Lohan, Bon Jov na wasanii wote wa kundi la Destiny Child, kundi pendwa la wakati wote kwa Mutassim.

Tom anasema mahusiano ya Mutassim na Beyonce ni ya muda mrefu kwani mwaka 2007, kulikuwa na Party ya siku yake ya kuzaliwa na Mutassim alikuja hapo na kaka zake na wageni waalikwa, Beyonce alitumbuiza pia. Siku hiyo pia baada ya show watu walitawanyika ila Beyonce na Mutassim waliingia gari moja haijajulikana walienda wapi.

Mwaka 2009 kulikuwa na tetesi kuwa ukaribu wao, ulivuka mipaka na watu kuhisi wameshatoka kimapenzi lakini kama ujuavyo, maisha huenda kasi si unajua mapenzi yalivyo na nguvu, jamaa akasahau kuwa ni mshauri wa usalama wa Baba yake na mwaka 2010-11 vugu vugu la mapinduzi likaanza kwa shinikizo la nchi za Magharibi.

Mutassim aliamini kuwa hakuna nchi ingeweza kumng’oa madarakani baba yake, kwanza ndani ya nchi ya Libya walijenga maeneo mengi ya nyumba za kujificha, pia yeye na mzee wake wakakataa kabisa kuishi nje ya Libya waliahidi kuwa watafia Libya.

Oktoba 20 2011, Masaa machache baada ya Mzee Gaddafi kuuawa, Mutassim naye akakamatwa na Waasi akiwa amechoka mbaya huko mjini Sirte na usiku huo huo alipelekwa mjini Misrata, akauawa na kuzikwa kwa siri Jangwani mpaka leo kaburi halijulikani lilipo kwani walimpeleka mbali, ili wasahau kabisa uzao wa Gaddafi.

Kabla hajauawa aliulizwa, “mlikuwa unaishi kwa raha sana na kutukandamiza sisi tulio wengi, tuambie sasa baba yako yuko wapi?” Mutassim aliwajibu waasi hao kwa kusema, “naomba maji ya kunywa” kisha akatoa sigara yake mfukoni na kuanza kuvuta halafu akasema “kama baba yangu (Gaddafi) kawafanyia mabaya ndugu zake wa Libya basi ikiisha hii sigara niuweni,” Mutassim akauawa kwa risasi ya shingo.

Baraza azipeleka Simba, Young Africans nusu fainali
Simulizi: Utamu wa pesa za Bangi ulivyonipa tiketi ya kwenda Jela