Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Francis Baraza amesema Simba SC na Young Africans, zina nafasi kubwa za kutinga Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku akizitaka kujipanga kikamilifu.

Simba SC na Young Africans zimewafahamu wapinzani wao katika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya kupangwa kwa Droo juzi Jumanne (Machi 12) mjini Cairo, Misri.

Simba SC imepangwa kukutana na Mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri, huku Young Africans wakipewa Mabingwa wa Soka Afrika Kusini Mamelodi Sundown.

Kocha Baraza amesema amekuwa mfuatiliaji mzuri wakati timu za Simba SC na Young Africans zinapocheza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa, na ameona timu hizo zina nafasi kubwa ya kufanya vizuri.

Amesema kinachotakiwa kufanywa na Mabenchi la Ufundi ya timu hizo ni kujiandaa vizuri huku yakiweka mikakati madhubuti ya kupambana katika michezo yote ya nyumbani na ugenini.

“Nimecheza na Simba SC na Young Africans kwenye mechi za Ligi Kuu, pia nimefuatilia timu zao pinzani, kwa maana ya Mamelodi Sundowns na Al Ahly, zinafungika ni makocha kufanyia marekebisho kwenye vikosi vyao,”

“Young Africans ina kikosi kizuri, hivyo ina uwezo wa kupambana na hao Mamelodi Sundowns, lakini vile vile Simba SC imecheza mara nyingi na Al Ahly, ikicheza nyumba wafunge mabao dakika za mwanzo angalau mawili na kuendelea, naiona hatua ya kutinga Nusu Fainali.” amesema Baraza

Jambo lingine alilolizungumzia Baraza ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, kushirikiana na klabu za Simba SC na Young Africans ili ziweze kufanikiwa kupata ushindi zitakapocheza nyumbani.

“TFF ni muhimu kuziunga mkono klabu hizo, ili ziweze kufanya vizuri, zinapocheza uwanja wa nyumbani na hilo linawezekana,” amesema

Al Ahly wamrudisha fasta Benchikha
Makala: Kifo cha fedheha cha mtoto wa Rais Mtanashati