Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dkt. David Mathayo ameishauri Serikali kuangalia gharama za uunganishaji umeme kwa Wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotambulika kama Vijiji Miji, ili kuwawezesha Wananchi wengi kuunganisha umeme kwenye maeneo yao.

Ameshauri kuwe na usawa wa gharama za uunganishaji umeme kati ya wananchi wa vijijini na Vijiji Miji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.

Dkt. Mathayo ameyasema hayo Mkoani Pwani wakati wa kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme Vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini – REA, Mkoani Pwani akiambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio .

Kwa upande wake Naibu Waziri Kapinga amewashauri wakazi wa vijijini kutumia umeme kwa shughuli za maendeleo na kuchangamkia uunganishaji wa umeme kwenye maeneo yao mara baada ya Serikali kufikisha miundombinu ya umeme akisema wakazi wa Vijijini hulipia gharama za umeme wa REA kwa shilingi 27,000 baada ya Serikali kulipia gharama nyinginezo, huku wakazi wa Vijiji Miji wakilipia shilingi 320,000 sawa na wakazi wa mijini.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alitoa rai kwa wananchi Vijijini kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya chini kwani Serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha umeme unafika kwenye maeneo hayo.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini – REA, Mhandisi Hassan Saidy alisema zaidi ya Shilingi Bilioni 44 zimetumika katika kutekeleza miradi ya REA na kufanikisha kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 100 kati ya vijiji 110 vilivyopo mkoani Pwani.

Makala: Sintofahamu ya Wosia tata wa Marehemu Elisabeth
Simulizi; Sitasahau niliyopitia kwenye kazi ya ulinzi