Homa ya pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji Simba SC dhidi ya Al Ahly imezidi kupamba moto baada ya Simba SC kuamua kujichimbia mapema Kisiwani Zanzibar kwa ajili ya mchezo huo wakiwa na sababu kuu mbili.

Klabu hiyo baada ya kucheza mechi zake mbili nyumbani dhidi ya Mashujaa ikishinda mabao 2-0 Singida Big Stars mabao 3-1, imeamua kwenda Zanzibar kuweka kambi.

Kocha Abdelhak Benchikha amesema aliuomba uongozi kuweka kambi Kisiwani humo kwa lengo la kupata wakati mzuri wa kufanya mazoezi usiku na sehemu tulivu.

Amesema kikosi kitakaa Zanzibar kwa siku saba hadi nane huku akiweka wazi kuwa watapata nafasi ya kucheza mechi moja ya kirafiki ili kufungua miili ya wachezaji baada ya mazoezi ya kujiweka fiti na tayari kwa mchezo.

“Sababu kubwa ya kuomba kambi kupelekwa Zanzibar kwanza kuna uwanda mkubwa wa kupata uwanja ambao utakuwa rafiki kwetu kufanya mazoezi usiku na tutafanya hivyo kwa muda ambao tunatarajia kucheza mchezo,” amesema na kuongeza;

“Pia nilihitaji utulivu wa kikosi, Zanzibar ni sehemu sahihi hasa wakati huu ambao ni mfungo, kule hakuna ligi inachezwa na ni wakati mzuri kwangu kukutana na wachezaji wangu wote kwa ajili ya mazoezi baada ya kupata futari na kupumzika tunajumuika pamoja.” amesema.

Akizungumzia kuhusiana na mchezo wa kirafiki, amesema hilo sio jukumu lake kutafuta timu lakini ameuomba uongozi ufanye hivyo kabla ya kurudi Dar es salaam kwa ajili ya mechi wawe wamecheza mchezo mmoja wa kirafiki.

“Programu yangu ni muhimu kwa mchezo mmoja kama tutakaa siku saba hadi nane hatuwezi kufanya mazoezi bila kufungua miili ya wachezaji kwa kucheza mchezo mmoja ambao hautahitaji nguvu nyingi kutumika nitakachoangalia zaidi ni namna wachezaji wameelewa kile nitakachowaelekeza na kufungua mili yao.” amesema Benchikha.

Alipotafutwa kuzungumzia msafara wa wachezaji walioenda Zanzibar, Meneja Habari na Mawasilino wa Simba SC, Ahmed Ally amesema ni wote isipokuwa walioitwa timu zao za taifa.

“Kikosi kinaondoka jana’ saa kumi na wachezaji wote kasoro wale walioitwa timu zao za taifa hivyo hatujaacha mtu Dar es salaam tumeenda tukiwa kamili kujiweka fiti kumkabili Al Ahly” amesema.

Alipoulizwa kuhusu mechi ya kirafiki amesema ni kweli itakuwepo lakini hakutakuwa na ruhusa ya mashabiki kushuhudia kuanzia mazoezi hadi mchezo wa kirafiki.

Mtoto apigiwa chepuo kurudi nyumbani
Bruno Guimaraes azigonganisha PSG, Real Madrid