Wakati mastaa wa Young Africans, Pacome Zouzoua na Khalid Aucho wakitarajiwa kuwa sehemu ya mchezo wa Jumamosi (Machi 30) dhidi ya Mamelodi Sundowns, mlinzi Yao Kouassi, hatokuwa sehemu ya mchezo huo.

Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika  dhidi ya Mabingwa hao wa Afrika Kusini, mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam kuanzia saa 3.00 usiku.

Daktari wa Young Africans, Moses Etutu amesema Aucho anaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi anaamini kabla ya Jumamosi (Machi 30) atakuwa fiti, lakini Kouassi atalazimika kukaa nje ya dimba kwa wiki tatu zaidi.

Amesema kwa upande wa Pacome ambaye aliumia goti, wanasubiri ripoti kutoka timu yake ya taifa ya Ivory Coast ambayo imeweka kambi nchini Ufaransa.

“Aucho tayari anaendelea vizuri na tuna matumaini naye kama ilivyokuwa kwa Pacome ambaye pia anaendelea vizuri kwa mujibu wa vipimo vya awali lakini kabla ya kumtumika katika mchezo wa Jumamosi (Machi 30) tunapaswa kuangalia vipimo ya mwisho,'” amesema.

Amesema kwa upande wa Kouassi bado anatakiwa kuendelea kuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu kutokana na kuchanika nyama za paja.

Daktari huyo amesema mchezaji ambaye kwa asilimia kubwa hawezi kuwa sehemu ya mchezo huo ni Kouassi pekee, wengine wana matumaini makubwa watatumika kulingana na uhitaji wa Benchi la Ufundi, hivyo mashabiki wanatakiwa kuwa na amani.

Young Africans na Mamelodi Sundowns zinakutana kwa mara ya pili, baada ya mwaka 2001 kukutana katika Raundi ya Pili ya michuano hiyo.

Young Africans walianzia nyumbani ambapo mchezo wa kwanza walikubali kipigo cha mabao 3-2 kabla ya kwenda ugenini na kutoka sare ya mabao 3-3.

Timu hiyo ambayo ina maskani yake Mitaa ya Twiga na Jangwani, imefika hatua ya Robo Fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi D, ikiwa na alama nane nyuma ya Al Ahly ya Misri yenye alama 11.

Shaka awa Mbogo mapungufu ujenzi wa Hospitali Kilosa
MAKALA: Usishangae ni uhalisia wa Mwanaume