Majira ya saa 10:15 alfjiri huko Bonde la Ruvu, Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mkoa wa Pwani, Katika Barabara ya Morogoro – Dar es Salaam Basi lenye namba za usajili T668 DTF aina ya Scania Kampuni ya Sauli, likiendeshwa na dereva Idd Aloyce (35), mkazi wa Mafinga, likitokea Dar es Salaam kuelekea Mbeya, liligonga ubavuni lori la mafuta ya Petroli.

Lori hilo lenye namba za usajili RAF672N na tela lenya namba RL2594 aina ya Howo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Rwanda likiendeshwa na dereva, Mushimana Musiyimana lilikuwa limesimama kupisha gari lililokuwa linakuja mbele yake.

Basi la hilo la Sauli, lilikuwa limeongozana na basi la Kampuni ya New Force liitwalo Golden Deer lenye namba za usajili T175 DZU, likiendeshwa na dereva Burton Jacob (33), mkazi wa Mbeya ambapo nalo lililigonga kwa nyuma basi la Sauli lililokuwa mbele yake.

Katika ajali hiyo, vilitokea vifo vya watu wawili ambao hawakufahamika majina yao mara moja na watu watatu walijeruhiwa ambao ni Salimu Daud (50), mkazi wa Mbozi, Farida Idrisa (26), mkazi wa Tabata Dar es Salaam na Kiambile Geofrey ambaye ni mkazi wa Uyole Mbeya.

Baada ya ajali hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wakiwa katika harati za kuwatoa marehemu waliokuwa wamenasa kwenye gari ghafla magari hayo yaliwaka moto uliotokana na Petroli iliyokuwa inavuja toka kwenye tenki la mafuta.

Walifanikiwa kudhibiti moto huo na kuwatoa marehemu ambao walikuwa wameteketea kwa moto, ndipo kwa mara nyingine moto ulilipuka tena toka kwenye moja ya chumba cha tenki la mafuta na kusababisha majeraha kwa Askari wawili wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji ambao ni Koplo Hamis Kungwi na Koplo Elias Bwire waliokimbizwa Hospitali ya Mloganzila kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

Akiongea na vyombo vya Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wa mabasi yote mawili, kushindwa kuchukua tahadhari kwa kuyapita magari mengine, lakini pia kushindwa kutunza umbali kati ya gari moja na lingine wakati yakiwa yanafuatana safarini.

Alisema, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya injini ya basi la Sauli iliyokuwa imekita chini baada ya kugonga gari lingine na kulipua Petroli wakati wa uokoaji.

Baada ya ajali hiyo, Mkuu wa mkoa wa Pwani. Abubakari Kunenge alitembelea eneo la tukio na kusema atayafungia kupita Mkoa wa Pwani mabasi yatakayoendelea kuvunja Sheria za Barabarani katika Mkoa huo.

Endelea kuangalia Picha za matukio mbalimbali mara baada ya ajali hiyo.

 

WITO:

Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani, limewataka madereva kutii sheria za usalama barabarani kwa mujibu wa taaluma zao, na kusema madereva hao wanachukua dhamana kubwa ya maisha na mali za watu huku likiwasisitiza Wananchi kuwa na tahadhali kubwa katika majanga ya moto, kwani wanatakiwa kuwa umbali wa mita 200.

USALAMA BARABARANI NI JUKUMU LETU SOTE.

Serikali yaahidi kuifanyia kazi ripoti ya CAG
Bodi ya ETDCO ivunjwe - Dkt. Biteko