Simba SC imeelekeza nguvu kwa sasa katika michuano ya Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu huku Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha akiachiwa kazi ya kuanza kusuka upya kikosi kwa msimu ujao, lakini akiwa na kibarua zaidi eneo la beki ya kati baada ya Henock Inonga na Che Malone kudaiwa wapo mbioni kusepa.

Awali iliwahi kudokezwa kuhusu taarifa za Inonga kujiandaa kuondoka kikosini hapo, akidaiwa kuwindwa na Far Rabat inayonolewa na kocha wa zamani wa Young Africans, Nasreddine Nabi, lakini taarifa zaidi zinasema hata Che Malone naye yupo njiani kusepa na ameanza kuaga klabuni.

Inaelezwa, ghafla tu Che Malone Fondoh ameshtua baada ya kuwaambia marafiki zake mwisho wa msimu huu ataondoka Simba SC.

Malone aliyetua kikosini msimu huu akisaini mkataba wa miaka miwili amewaambia marafiki zake wa karibu ikiwemo wakala wake, amtafutie timu nyingine kwani anataka kufanya makubwa zaidi kabla ya kustaafu.

Hata hivyo, beki huyo aliyetua Simba SC akitokea Cotonsport ya Cameroon amethibitisha hilo katika mahojiano na kituo cha Canal- Sports cha Ufaransa kupitia kipindi maalumu kinachohusu soka na wachezaji wa Afrika, akisema anafikiria kuondoka Simba SC mwisho wa msimu.

“Nilicheza Cotonsport kwa misimu miwili na kutwaa taji la Ligi mara mbili mfululizo, nikataka kupata changamoto mpya. Nacheza soka ili kupata maendeleo na sio kubaki katika eneo moja tu.” amesema Malone na kuongeza

“Ndoto yangu ni kucheza kwenye klabu kubwa na naamini msimu ujao nitakuwa timu kubwa, kwenye soka miujiza pekee ni nidhamu na kufanya kazi kwa bidii. Simba SC ni hatua nyingine kwangu kwa kuwa ndoto yangu ni kucheza kwenye moja ya klabu kubwa duniani.” amesema Che Malone

Meneja Habari na Mawasilino wa Simba SC, Ahmed Ally alipoulizwa juu ya taarifa hizo amesema kwa sasa timu inajali zaidi michezo inayofuata ukiwemo wa kesho Jumanne (Aprili 09) wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Mashujaa hivyo jambo la kusajili au kuondoka kwa wachezaji wapya limeachwa kwa kocha ndiye atafanya maamuzi.

Usajili wote tumemuachia kocha, yenye ndiye ataamua nani aondoke au kubaki kikosini kutokana na aina ya timu anayoitaka kwa msimu ujao hivyo hayo tuayaache kwanza tuzingatie zaidi mechi zijazo, alijibu Ahmed alipoulizwa kuhusu suala hilo.

Kama Malone na Inonga wataondoka Simba SC kwa pamoja, basi timu hiyo itatengeneza pesa ndefu kutokana na thamani ya kuwang’oa kikosini hapo kutokuwa chini ya 600 milioni kwa kila mmoja lakini itapata kibarua cha kuingia sokoni kushusha majembe mapya yatakayoziba nafasi zao.

PSG imedhamiria kwa Victor Osimhen
Rais Young Africans atoa la rohoni