Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imepokea dozi 500,000 za Chanjo ya Sinopharm kutoka Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ikiwa ni msaada unaotokana na ushirikiano bora baina ya nchi hizo mbili.
Shehena hiyo imepokelewa leo Novemba 1, 2021 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima aliyeambatana na viongozi wengine wa kitaifa na Mkoa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.
Katika tukio hilo Dkt. Gwajima ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa ushirikiano wanaoendelea kuonesha ikiwa ni pamoja na kusaidia kuboresha sekta ya Afya nchini ikiwemo katika mapambano dhidi ya magonjwa mbali mbali ikiwemo ugonjwa wa UVIKO-19.
“Shukrani za pekee ziwaendee serikali China hususani katika kujali afya za Watanzania kwa kutupatia Chanjo hizi aina ya Sinopharm Dozi 500,000 ambazo zitatusaidia kuwakinga watanzania 250,000 dhidi ya mapambano ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona (UVIKO-19).” Amesema Dkt. Gwajima.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini sana afya za Watanzania. Ndiyo maana tumeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za kinga nchini. Amesisitiza Dkt. Gwajima.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali ilipata jumla ya Chanjo Dozi 1,058,400 aina ya Janssen (Johnson and Johnson) ambazo zilishaisha na Sinopharm Dozi 1,065,600 kutoka shirika la COVAX ndiyo hivi sasa zimeendelea kutolewa katika vituo vyote nchini na kupitia huduma ya mkoba na kusisitiza, wananchi wote, wenye miaka 18 na kuendelea waendelee kupata huduma hiyo.
Aidha Dkt. Gwajima amesema, Wizara ilitoa mwongozo wa chanjo unaofafanua vyema taratibu za utoaji wa chanjo hizi wenye lengo la kufikia uchanjaji wa asilimia 60 ya watanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.
“Wizara ilitoa mwongozo wa chanjo unaofafanua vyema taratibu za utoaji wa chanjo hizi wenye lengo la kufikia uchanjaji wa asilimia 60 ya watanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.” Amesema.
Pia, Dkt. Gwajima ameipongeza mikoa mitano ambayo inaongoza kwa kasi ya utoaji wa chanjo ya Sinopharm ambayo ni Ruvuma, Mbeya, Mtwara, Dodoma na Kagera.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Jamii nzima kujitokeza kupata chanjo hii dhidi ya UVIKO-19 ili kupunguza milipuko ambayo inaweza kutokea mara kwa mara na kuepuka madhara makubwa kama kifo na kulazwa kwenye oksijeni kwa muda mrefu.