Utunzaji wa vyanzo vya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, umesaidia kuwatua Wanawake ndoo kichwani kijijini Mshabaigulu kata ya Kihanga wanaopata huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa wakala wa Maji safi na salama vijijini – RUWASA.
Mradi huo uliogharimu Shilingi 497 milioni na unaoenda kuwahudumia wananchi zaidi ya 2000 unapatikana kilomta 10 kutoka chanzo hicho kilipo.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila pamoja na mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Laizer na viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wakikagua chanzo cha maji, kijiji cha Mshabaigulu.
Akizungumza katika ziara yake ya siku tatu ya kutembelea miradi kwenye halmashauri ya Karagwe, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amewasisitiza wananchi hao pamoja na wafugaji wa ng’ombe kuendelea kutunza vyema vyanzo vya maji kwani itawasaidia kupata uhakika maji safi na salama kupitia mradi huo na vyanzo vingine vya maji.
Amesema, “nyie wananchi mmetoa mchango mkubwa wa kutunza chanzo cha maji, kwahiyo niendelee kuwahasa kwamba mkoa wetu wa Kagera bado una wafugaji wengi na mara nyingi wafugaji ambao hawaijui kesho ni watu ambao huwa wanapenda kuharibu vyanzo vya maji.”
Kaimu Meneja wa RUWASA, Wilaya ya Karagwe, Juston Mtabuzi ameeleza mkakati uliopo wa kuendeleza na kutunza chanzo cha maji hicho ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo.
Amesema, “Maji haya yatumike kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kwahiyo umuhimu wa utunzaji wa vyanzo ndio unatusaidia sisi kutoa huduma, tumekwisha shuhudia maeneo mengi mradi unakuwepo alafu chanzo kinapotea kwasababu ya shughuli za kibinadamu.”
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila akimtua ndoo kichwani mama wa kijiji cha Mshabaigulu.
Kwa upande wao wananchi wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo kwani awali walikuwa wakitumia maji kwa pamoja na mifugo na walikuwa wakitumia umbali mrefu kupata hitaji hilo.
Ujenzi wa mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili, 2022 na kukamilika Septemba 29, 2022 kwa gharama ya Shilingi 497 milioni.