Kiungo na nahodha wa FC Barcelona Andres Iniesta amesaini mkataba wa kudumu ambao utamuwezesha kuendelea kuitumikia klabu hiyo katika maisha yake yote ya soka.

Iniesta amejitoa muhanga kwa kufanya maamuzi hayo mazito, baada ya kuwa na mazungumzo kwa kipindi cha muda mrefu na viongozi wa FC Barcelona ambayo yalilenga kumsainisha mkataba mpya.

Katika mazungumzo hayo suala la kumtaka kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 kusalia klabuni hapo kwa kipindi cha maisha yake yote, liliibuliwa na alikubaliana na ombi hilo.

Hii inamaanisha Iniesta ataendelea kuwepo Camp Nou hata kama atatangaza kustaafu kucheza soka siku za usoni, ambapo mkataba wake utamuwezesha kukabidhiwa majukumu mengine klabuni hapo.

“Andres Iniesta amesaini mkataba wa maisha na FC Barcelona leo ijumaa, mkataba huu utamuwezesha kuwepo klabuni hapa katika kipindi chote cha maisha yake.

“Tangu mwaka 2015 Iniesta amekua nahodha wa kikosi cha FC Barcelona, na maamuzi aliyoyachukua yanaendelea kumpa wasifu wa kipekee ndani ya klabu hii, ambayo ilimkuza tangu akiwa na umri mdogo.”

Mpaka sasa Iniesta ameshaifungia Barcelona mabao 55 tangu alipoanza kuitumikia timu ya wakubwa Oktoba 29, 2002.

 

 

Syria yajisogeza fainali za kombe la dunia 2018
Messi hatarini kukosa kombe la dunia 2018