Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kutumia mafunzo wanayopatiwa kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa Baraza la wafanyakazi katika kuweka mahala pa kazi kuwa sehemu salama katika utendaji wa kazi na kuhakikishakuwa wajumbe wa OWMS wanatekeleza majukumu waliyokasimiwa.

Dkt. Luhende ameyasema hayo hii leo Oktoba 12, 2022 wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wapya wa Baraza la Wafanyakazi wa OWMS yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma ambapo amesema kuwa mada tatu zitawasilishwa kwa wajumbe hao ikiwemo Wajibu na Majukumu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, kupitia Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi; na Umuhimu wa Baraza la wafanyakazi mahala pa kazi.

Amewataka wajumbe kutumia fursa hiyo kuzijua hadidu za rejea ambazo zitawaongoza katika utendaji kazi wa kila siku na kutekeleza majukumu katika kipindi chote cha miaka mitatu watakachokuwa wajumbe wa Baraza hilo kuwa nguzo kati ya Baraza na watumishi wengine kwa kuwa Baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu mahala pa kazi na kuwa sehemu salama ili kuleta tija katika utendaji kazi wa kila siku wa OWMS na amewataka wajiandae kuhamia Dodoma mwaka huu.

“Mada inayohusu Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi ni mahususi kwa ajili ya kujenga uwezo na maarifa ya kujua kilichopo katika mkataba wetu kati ya Menejimenti na Baraza hili ikiwemo matarajio ya OWMS kutoka kwa wajumbe ukizingatia kuwa mkataba huu ni nyenzo muhimu kabisa katika utendaji kazi wetu kwa sababu unaainisha majukumu na mipaka yetu na matarajio kutoka kwa wafanyakazi,” amesema Dkt. Luhende.

Akitoa mada ya Umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samuel Nyungwa amesema kuwa ni muhimu kwa kila mtumishi kujiunga na chama cha wafanyakazi kwa sababu ni taasisi pekee ya wafanyakazi ambayo imeundwa kwa ajili ya kulinda na kutetea haki kwa kuweka sawa mahusiano ya kazi kati mfanyakazi na mwajiri wake mahali pa kazi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemarila Rutatina amesema kuwa mkataba wa Baraza la Wafanyakazi unaleta mafanikio na ushirikiano mahala pa kazi kwa kuwa unawaweka pamoja na kuwaleta karibu watumishi mahali pa kazi.

Mwanajeshi mbaroni kwa kuuza risasi kwa wahalifu
BRELA yaja na dawa ya Matapeli