Kocha Mkuu wa Simba SC Mualgeria, Abdelhak Benchikha amesema kwa sasa jambo kubwa analofanyia  katika kikosi hicho ni kujenga wachezaji wa timu hiyo kisaikolojia kabla ya kucheza mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Benchikha amesema hakuna jambo kubwa atakalolifanya kwa muda mchache uliobaki ingawa atakachopambana nacho ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji ili waweze kupata matokeo mazuri ugenini.

“Nafurahi kufanya kazi katika klabu hii kubwa hapa nchini na malengo yangu ni kuona inapiga hatua kama ambavyo nimefanya kule nilikotoka, kuhusu mpango wa mechi siwezi kuweka wazi bali nitaendelea na ripoti ya watangulizi waliopo,” amesema.

Aidha Benchikha ameongeza ili timu hiyo ipige hatua inahitaji ushirikiano mkubwa kuanzia kwa viongozi na wachezaji kwani hilo ndilo jambo kubwa litakalowafanya kufika katika malengo yao waliyojiwekea licha ya yeye kuingia katikati ya msimu

Benchikha alitangazwa rasmi kukiongoza kikosi hicho Novemba 24, mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili akichukua nafasi ya Mbrazili, Roberto Oliveira Robertinho’ aliyetimuliwa Novemba 7, baada ya kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Yanga.

Benchikha aliachana na klabu ya USM Alger ya kwao Algeria ambapo alitoka kuipa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Yanga na CAF Super Cup mbele ya Al Ahly ya Misri iliyotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Simba SC inakwenda katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi B, kwa kumiliki alama moja sawa na Asec Mimosas inayoshika nafasi ya pili, huku Jwaneng Galaxy ikiongoza kundi hilo kwa kuwa na alama tatu.

Wydad Casablanca ya Morocco inaburuza mkia wa Kundi B ikiwa haina alama yoyote, kufuatia kukubali kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy iliyokuwa ugenini.  

Mlipuko wa Kipindupindu waua 23, Mvua yachangia
Mkurugenzi, Watumishi wanusurika kifo ajalini