Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe kimewataka wananchi mkoani humo na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuulinda na kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa muda wa miaka 55 tangu Tarehe 26 April 1964.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Siasa na Uenezi mkoani humo, Erasto Ngole ambapo amesema kuwa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar ziliungana mwaka 1964 chini ya waanzilishi wake Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Abeid Karume ambao kwa pamoja walifanikiwa kuitengeneza nchi ya Tanzania.

“Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walifanikiwa kutuunganisha sisi tuliokuwa wa Tanganyika wakati huo na wenzetu wa Zanzibar Tarehe 26 Mwezi Aprili mwaka 1964 kisha ikapatikana nchi moja hii ya Tanzania ambayo tunafurahia sana uwepo wetu katika nchi hii,” amesema Ngole

Aidha, uongozi wa chama hicho umetoa wito kwa wananchi kuendelea kuulinda, kuuthamini na kuudumisha Muungano huo kwa kuzidi kuimarisha amani, umoja na mshikamano pamoja na kuwaombea pumziko la amani waasisi wa Muungano huo Mwl.Julius Nyerere na Abeid Karume ambao wametangulia mbele za haki.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe, Paza Mwamlima amesema kuwa Wananchi wa Tanzania wanakazi kubwa ya kuwaenzi waasisi hao wa Muungano kwa kufanya kazi zenye manufaa kwa pande zote mbili za Tanzania Bara na Visiwani ikiwa ni pamoja na kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano.

Ameongeza kuwa Tanganyika na Zanzibar tangu zilipoungana kuwa Tanzania zimekuwa chini ya utawala wa chama cha mapinduzi hivyo jambo hilo la Muungano litabaki kuwa la kihistoria katika Afrika na Dunia kwa ujumla na kuongeza kuwa kitendo cha waasisi hao kuchanganya udongo wa pande mbili ni ishara tosha ya kudumisha na kuulinda muungano huo.

Baadhi ya Wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani Njombe wameeleza faida wanazozipata kutokana na uwepo wa Muungano huo wa nchi mbili kuwa ni pamoja na fursa za kibiashara, kazi na elimu kwakuwa mambo hayo hayana mipaka wala masharti magumu pindi wananchi wapande hizo mbili wanapotaka kufanya shughuli zao upande mmoja wapo.

 

Error: Contact form not found.

Video: Sugu amuomba kazi Rais Magufuli, aeleza anavyomuunga mkono
LIVE: Ziara ya Rais Magufuli mkoani Mbeya | Akihutubia Taifa