Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo amezindua kituo cha kwanza cha kisasa cha kujazia gesi asilia kwenye magari na karakana ya kuweka mfumo wa gesi asilia ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa mipango ya Serikali kuchochea matumizi ya gesi asilia kama nishati safi na salama kwa mazingira.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam Novemba 11, 2023 na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Balozi Sherif Ismail wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Balozi Isaac Njenga wa Jamhuri ya Kenya, Balozi Fred Mwesigye wa Jamhuri ya Uganda, Mha. Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya TAQA, Pakin Kafafy.
Dkt. Biteko amesema, kujengwa kwa kituo hicho na TAQA Arabia na washirika wao JCG Oil & Gas niutekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa na maono ya kuleta wawekezaji nchini wakiwemo wanaowekeza kwenye Sekta ya Nishati, hivyo ameahidi kuwa Wizara itafanyia maelekezo yake ili kutekeleza maono yake.
Amesema, Serikali inaweka msukumo mkubwa kwenye matumizi ya gesi ya asilia yakiwemo magari, mitambo ya viwandani, hivyo kuzinduliwa kwa kituo hicho ni kuonesha azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa Gesi inayopatikana Tanzania inatumika ndani ya nchi kwanza.
Kituo hicho kitajaza gesi kwenye magari 800 kwa siku na kina pampu sita zitakazojaza gesi kwenye magari sita kwa maramoja ambapo ujazaji wa gari moja utakuwa ni wa dakika tatu hivyo hicho ni kituo kikubwa kitakachosaidia kubadilisha magari na kufanya yatumie gesi badala ya mafuta pekee.
Aidha, Dkt Biteko amesema Kampuni hiyo inatarajia kujenga vituo 12 vya CNG jijini Dar es Salaam ili kuwa na vituo vingi zaidi vya kujazia gesi kwenye magari na kwamba na kwamba Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika uwekezaji wao ili kuchochea ukuaji wa nishati nchini.
Ameongeza kuwa, kampuni hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wapo kwenye majadiliano ili kujenga vituo vidogo vya Gesi ya Kusindika (LNG) ili kuweza kutoa Gesi jijini Dar es Salaam na kupeleka kwenye mikoa mbalimbali ili nayo iweze kujaza gesi hiyo kwenye magari..
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya usambazaji nishati katika maeneo yote ikiwemo gesi asilia.
Amesema kuwa Wilaya hiyo inaona faraja kufunguliwa kwa kituo wilayani humo kutokana na kuwa kitovu cha Mkoa wa Dar es Salaam kwani Wilaya hiyo ina wananchi wasiopungua milioni 1.6 ukilinganisha na idadi yote ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao jumla yao ni milioni 5.3.