Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.
Majaliwa ameyasema hayo, kufuatia muendelezo wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), wa kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu kwa kuwapatia mafunzo kazini kuzaa matunda baada ya kampuni hiyo kuibuka mshindi wa pili katika tuzo zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Amesema, anawapongeza GGML kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo, uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi huku akitoa wito kwa waajiri wote kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa.
Kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu (2023), inayosema “Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Uzalishaji wa Wafanyakazi Wenye Ujuzi Nchini Tanzania”, Waziri Mkuu alisema ni thabiti kwani inaweka msisitizo katika ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.
Awali, akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Meneja Mwandamizi Rasilimaliwatu wa GGML, Charles Masubi aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika uzalishaji wa vijana bora wanaokubalika katika soko la ajira.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Makakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujuzi wa Mwaka 2016/17-2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri, wadau, vyuo au taasisi za elimu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania -ATE, Suzanne Ndomba-Doran alisema ili Tanzania iweze kushiriki kikamilifu katika soko shindani la Afrika Mashariki na dunia ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe katika kukuza ujuzi hususani kwa vijana.
GGML, ilibeba tuzo katika kundi la waajiri wakubwa kutokana na mchango wake wa uzalishaji wa rasilimaliwatu wenye ubora kwa soko la ajira, ikiwa nisiku chache baada ya kupokea wahitimu 50 (30ke / 20me), toka vyuo vikuu mbalimbali nchini ambao wameanza kupatiwa mafunzo kazini na kwa mwaka jana vijana 26 walihitimu mafunzo kama hayo.