Gari la Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko limemgonga Mtumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, Moses Mjuni na kufariki dunia papo hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Khadija Nyembo amesema kuwa ajali hiyo imetokea saa mbili usiku ambapo Gari la Mbunge huyo lilimgonga Mtumishi wa Hospitali ya Magu ambaye alikuwa anaendesha pikipiki na dereva wa gari hilo teyari ameshakamatwa na Jeshi la Polisi.

Aidha, kwa upande wake, Esther Matiko amesema kuwa ajali hiyo imetokea takribani kilomita 10 kutoka daraja la Mto Simiyu wakati akitokea Mwanza.

“Nilitoka Mwanza saa 12:00 jioni kwenda Jimboni kwangu (Tarime), tulipopita mbele kidogo karibu kilomita 10 kutoka Daraja la Mto Simiyu, ghafla alitokea mwendesha pikipiki akiwa ana yumba yumba na dereva alishindwa jinsi ya kumkwepa akamgonga, mimi nilikuja kuona yule mtu teyari ameshakufa,”amesema Mtiko.

Hata hivyo, Matiko amesema kuwa alikuwa anajisikia maumivu makali ya mgongo na mbavu hali ambayo ilimlazimu kufanyiwa vipimo kuona kama amepata madhara.

Trump agomea dhifa iliyoandaliwa na waandishi wa habari nchini Marekani
Mahakama kuu Zanzibar yamhukumu kunyongwa askari Polisi