Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22 George Mpole huenda akaendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Geita Gold FC msimu ujao, kufuatia mipango na taratibu zinazoendelea kuchukuliwa na Uongozi wa klabu hiyo ya mkoani Geita.

Mpole alikua anahusishwa na mpango wa kuondoka klabuni hapo, kufuatia uwezo wake wa kupachika mabao kuziamsha klabu kadhaa za Ligi Kuu na kutamani kumsajili katika kipindi hiki cha usajili.

Awali Mshambuliaji huyo alikua akitajwa katika mawindo ya vilabu vitatu vya jijini Dar es salaam (Simba SC, Young Africans na Azam FC), lakini mpango huo unaonekana kufa rasmi, kutokana na viongozi wa vilabu hivyo kufanya usajili wa Washambuliaji wengine kutoka nje ya nchi.

Kocha Mkuu wa Geita Gold FC Fred Felix Minziro aliwahi kusema kuwa, kutokana na kiwango kilichoneshwa na Mpole, huenda wangemkosa msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, kutokana na kuwindwa na klabu nyingi.

Hata hivyo Uongozi wa Geita Gold uliwahi kusisitiza kuwa, utapambana kumshawishi Mshambuliaji huyo kuendelea kuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao, kwa kuwa bado wanahitaji huduma yake katika Michuano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kwenye usiku wa Mastaa Mshambuliaji huyo alipewa tuzo ya Mfungaji Bora na alikua kwenye kikosi Bora cha msimu wa 2021/22.  

Haji Manara atupwa JELA miaka miwili
Simba SC, Vipers SC zamaliza sakata la Manzoki